UTURUKI

Kiongozi wa kundi la waasi la PKK nchini Uturuki Abdullah Ocalan atangaza kusitishwa kwa vita

Kiongozi wa kundi la waasi la Kikurdi nchini Uturuki anayekitumikia kifungo cha maisha jela Abdullah Ocalan amewataka waasi wa PKK kuweka silaha chini na kuacha vita dhidi ya serikali.

Matangazo ya kibiashara

Ocalan amewataka pia wapiganaji wenzake kuondoka nchini Uturuki ujumbe ambao umepokelewa kwa furaha kubwa na maelfu ya raia nchini humo waliokuwa wanaadhimisha mwaka mpya wa kabila la Kikurdi mjini Diyarbakir.

Mazungumzo kati ya waasi hao wa PKK yamekuwa yakiendelea na serikali ya Uturuki kumaliza makabiliano hayo ya zaidi ya miaka 30 dhidi ya serikali na kusababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 40.

Awali, juhudi za kusitisha mapigano kati ya kundi hilo lenye makao yake Kusini Mashariki mwa Uturuki yalikosa kuzaa matunda lakini wakati huu raia wengi nchini humo wanasema kuwa matumaini ni makubwa ya mapigano hayo kumalizika kutokana na mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan na kiongozi wa kundi hilo Abdullah Ocalan ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa sasa.

Kiongozi wa kundi hilo Ocalan licha ya kufungwa maisha jela na ambaye tayari amekitumikia kifungo cha miaka 14 anaaminiwa kuwa na ushawishi mkubwa na usemi wa mwisho ndani ya kundi hilo.

Ocalan ameongeza kuwa wakati wa kuweka silaha chini ni sasa na siasa na mawazo yanastahili kuchukua nafasi ili kuanza mapambano mapya ya demokkrasia.

Kundi hilo la PKK lililoanza mapambano yake rasmi mwaka 1984 dhidi ya serikali ya uturuki limekuwa likiangaziwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kama kundi la kigaidi.

Asilimia 20 ya raia wa Uturuki wanatoka katika kabila la Kikurdi.