UCHINA-URUSI

Rais mpya wa China Xi Jinping aanza ziara ya siku tatu nchini Urusi

Rais mpya wa China Xi Jinping amefanya ziara yake ya kwanza nchini Urusi kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili na kutia saini mikataba ya pamoja kuhusu nishati na uwekezaji.

Matangazo ya kibiashara

Rais Jinping atakuwa nchini humo kwa ziara ya siku tatu na anatarajiwa kuingia katika makubaliano hayo ya kibiashara na rais Vladimir Putin ili kuiwezesha Urusi kuanza kusafirisha mafuta yake nchini china taifa ambalo ni la pili kwa ukubwa kiuchumi duniani baada ya Marekani.

Rais Vladimir ameisifu China kwa kuendelea kuwa mshirika wake wa karibu katika maswala ya kiuchumi na siasa ,ushirikiano aliosema utaendelea kushudiwa na kudumu katika zijazo.

China na Urusi zimekuwa zikiungana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga azimio lolote dhidi ya serikali ya Syria kutoka kwa nchi za Magharibi dhidi ya rais Bashar Al Assad.

Baada ya ziara hiyo ya rais Jinping nchini Urusi,rais huyo anatarajiwa kuzuru barani Afrika na kukutana na viongozi nchini Tanzania, Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akiwa barani Afrika, rais Jinping atatumia fursa hiyo kuuza sera za China barani humo na kuimarisha biashara kati ya China na Afrika ikiwemo miradi ya uwekezaji.