Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy afunguliwa mashtaka kwa kujipatia fedha haramu
Rais wa zamani wa Ufaransa Nikolas Sarkozy amefunguliwa mashtaka ya kuendesha kampeni zisizosafi kwa kujipatia fedha kinyume cha sheria wakati akiwania urais mwaka 2007.
Imechapishwa:
Ofisi ya Mwendesha mashtaka wa serikali imesema kuwa ina ushahidi wa kutosha kudhibitisha mashtaka yanayomkabili Sarkozy na kwamba alitumia madaraka yake kama rais kujipatia fedha toka kwa mfanyabiashara tajiri, L'Oreal heiress Liliane Bettencourt.
Akisomewa mashtaka yake kwenye Mahakama moja mjini Paris, Mwendesha mashtaka wa polisi amesema kuwa Sarkozy na timu yake ya kampeni walijipatia fedha kienyeji kutoka kwa mwanamama huyo ambaye sasa afya yake inaelezwa kuzorota kutokana na kupoteza kumbukumbu.
Sarkozy amesisitiza kuwa alienda nyumbani kwa Liliane Bettencourt kumtembelea mume wake wakati wa kampeni na kwamba hakwenda kudai fedha kwa ajili ya kufadhili kampeni ya chama chake cha UMP, kauli ambayo inajikanganya na ile iliyotolewa na viongozi wa chama chake.
Makachero wanadai kuwa zaidi ya Euro milioni nne zilichukuliwa kutoka kwa Liliane Bettencourt kwa lengo la kufadhili kampeni zake jambo ambalo ni kinyume cha sheria za uchaguzi za nchi hiyo .
Tangu kushindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Sarkozy amekuwa akikabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo kutia saini mikataba mibovu ya kuuziana silaha na nchi ya Pakistan pamoja na matumizi mabaya ya ofisi katika kipindi chake cha utawala.