ICC-RWANDA-HAGUE

Bosco Ntaganda aondoka Kigali kuelekea Hague

Kiongozi wa makundi ya uasi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bosco Ntaganda  aliyejisalimisha kwenye Ubalozi wa Marekani mapema juma hili nchini Rwanda, ameondoka jijini Kigali kwenda Hague nchini Uholanzi katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC kufunguliwa mashtaka.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo amethibitisha kuondoka kwa Ntaganda jijini Kigali kuelekea Hague akiandamana na maafisa wa Mahakama ya ICC.

Baada ya kuwasili mjini Hague, Ntaganda atapimwa afya yake na baadaye Majaji wa Mahakama hiyo watapanga tarehe ya kuanza kusikiliza kesi dhidi yake na kwa muda huo wote atakuwa anazuiliwa katika Mahakama hiyo.

Hii ndio mara ya kwanza kwa mshukiwa wa ICC kujisalimisha kwenye Mahakama hiyo ya Kimataifa kutaka kushtakiwa kwa makosa ya ukiukwaji wa haki za bindamu anayotuhumiwa kutekeleza Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya mwaka 2002 na 2003 ambapo mamia ya watu walipoteza maisha.

Siku ya Ijumaa ujumbe kutoka Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC uliwasili mjini Kigali,  tayari kuanza mchakato wa kumsafirisha Ntaganda mjini Hague.

Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama hiyo Fatou Bensouda awali alithibitisha kuwa Ntaganda atafikishwa katika Mahakama hiyo hivi karibuni kufunguliwa mashtaka yanayomkabili.

Ntaganda anatuhumiwa kuongoza makundi kadhaa ya uasi Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya kupewa cheo katika jeshi la serikali kaa njiamojawapo ya kuleta amani Mashariki mwa nchi hiyo.