JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Waasi wa Seleka waanza safari ya kuelekea jijini Bangui baada ya kuuteka mji wa Bossangoa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Waasi wa Seleka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameanza tena makabiliano na wanajeshi wa serikali na wanaelekea jijini Bangui baada ya kuuteka mji wa Bossangoa siku ya Ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi nchini humo linasema kuwa waasi hao walianza harakati zao za kuuteka mji huo ulioko Mashariki mwa nchi hiyo siku ya  Ijumaa asubuhi baada ya kutangaza awali kuwa walikuwa na mpango wa kupambana na serikali kwa madai kuwa rais Francois Bozize alishindwa kutekeleza matakwa yao.

Msemaji wa kundi hilo la Seleka Eric Massi, amesema kuwa waasi hao wamefanikiwa kuchukua mji huo ulioko Kilomita 250 kutoka mji mkuu wa Bangui na sasa wanaelekea mjini humo.

Siku ya Jumatano juma hili, kundi hilo la waasi la Bangui lilitangaza kuwa lingerejea kukabiliana na wanajeshi wa serikali baada ya kudai kuwa makubaliano yaliyotiwa saini mjini Librevile nchini Gbaona kati ya kundi hilo na serikali mapema mwaka huu hayakutekelezwa.

Madai ya kundi hilo la Seleka yalikuwa ni kuitaka serikali chini ya rais Francois Bozie kuwaachilia huru wafungwa wote kutoka kundi hilo na kuhakikisha kuwa wanajeshi wa Afrika Kusini wanaondoka nchini humo.

Baada ya kitishio hicho, kutoka kwa kundi hilo rais Bozize aliamuru wafungwa wote wa kisiasa kuachiliwa huru na akatangaza kumalizika kwa hali ya hatari ya wiki 10 iliyokuwa imetangaza nchini humo kumalizika.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshtumu shambulizi lililotekelezwa hivi karibuni na waasi hao wa Seleka katika mji huo Bangassou jambo wanalosema linaweza kuendelea kuhatarisha hali ya usalama nchini humo.

Waasi wa Seleka walianza mpango wa kuiangusha serikali ya rais Bozize mwezi Desemba mwaka uliopita baada ya kuituhumu serikali ya Bangui kushindwa kutekeleza ahadi walizoafikiana kuhusu uongozi wa nchi hiyo mwaka 2007.