Wabunge nchini Cyprus wanapiga kura kuamua mpango wa Umoja wa Ulaya wa kubama matumizi ya fedha
Wabunge nchini Cyprus siku ya Ijumaa wanapiga kura kuamua mustakabali wa mpango wa Umoja wa Ulaya wa kubana matumizi ya fedha ili kulisaidia taifa hilo kujikwamua katika hali ngumu ya kiuchumi inayokabiliana nayo kwa sasa.
Imechapishwa:
Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya imeipa serikali ya Cyprus hadi Jumatatu ili kupata fedha za kuwasaidia kujikwamua kutoka kwa mdororo huo wa kiuchumi uliosababisha Benki nchini humo kufunga kwa muda.
Umoja wa Ulaya unasema ikiwa suluhu la haraka halipatikana basi Benki nchini humo zitakosa huduma kwa muda na kufungwa kwa kipindi kisichojulikana ili kuzuia wananchi kutoa fedha zote kwenye Benki hizo.
Waziri wa fedha wa Cyprus Michael Sarris, aliyekuwa amezuru Moscow kujaribu kupata usaidizi kutoka kwa Urusi ameondoka nchini humo baada ya kutopata mwafaka na viongozi wa nchi hiyo baada ya serikali ya Urusi kusema kuwa haukuridhishwa na mapendekezo ya Cyprus.
Cyprus inahitaji Euro bilioni 5 nukta 8 ili kupata mkopo wa Euro Bilioni 10 kutoka kwa Umoja wa Ulaya na shirika la fedha duniani IMF.
Wananchi wengi wa Cyprus ambao wana fedha katika akaunti zao wanahofia kuwa huenda serikali itatumia fedha zao kupata fedha za kupata mkopo wanaouhitaji ikiwa suluhu halipatikana haraka iwezekanavyo.