TANZANIA

Watu wawili wafa kufuatia kuanguka kwa jengo la ghorofa jijini Dar es Salaam Tanzania, rais Kikwete atembelea eneo la tukio

Wananchi wa Dar es Salaam wakishuhudia mabaki ya jengo ambalo limeanguka hii leo na kuua watu wawili
Wananchi wa Dar es Salaam wakishuhudia mabaki ya jengo ambalo limeanguka hii leo na kuua watu wawili Kwa hisani ya Ikulu ya Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametembelea eneo la tukio ambapo jengo la ghorofa kumi lilianguka leo asubuhi na kuua watu wawili huku wengine kadhaa wakihofiwa kunasa kwenye kifusi.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa vikosi vya uokoaji watu kumi na tano pekee ndio waliofanikiwa kuokolewa wakiwa hai.

Jengo hilo liliangua maajira ya sambili na dakika arobaini na tano ambapo watu wengi walikuwa wakiendelea na shughuli zao za kawaida kabla ya kusikika kishindo kikubwa kilichotokana na kuanguka kwa ghorofa hilo.

Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amethibitisha kufa kwa watu wawili kwenye ajali hiyo huku akisema ni watu kumi na tano pekee ndio wameokolewa wakiwa hai na kuongeza kuwa huenda kunawengine wamenaswa kwenye kifusi.

Vikosi vya uokoaji vinaendelea na juhudi za kuwaokoa watu wanaoelezwa kunaswa kwenye jengo hilo ingawa hakuna idadi rasmi ya watu ambao wanaelezwa pengine huenda walikuwa kwenye jengo hilo wakati linaanguka.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa huenda kukawa na watoto ambao wamenaswa kwenye kufusi kwakuwa wakati linaanguka walikuwa wakicheza jirani na jengo hilo.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadick Mecky Sadick amesema kuwa uchunguzi tayari umeanza kubaini chanzo cha kuanguka kwa ghorofa hilo na kwamba watu kadhaa wanahojiwa ambao ni wahusika waliokuwa wakisimamia ujenzi wake.