KOREA KASKAZINI-KOREA KUSINI

Rais wa Korea Kusini Park atangaza utayari wa nchi yake kuingia vitani dhidi ya jirani zao Korea Kaskazini baada ya kuchoshwa na vitisho vyao

Rais wa Korea Kusini Park Geun-Hye siku akila kiapo cha kuongoza Taifa lake na amesema wapo tayari kukabiliana kijeshi na Korea Kaskazini
Rais wa Korea Kusini Park Geun-Hye siku akila kiapo cha kuongoza Taifa lake na amesema wapo tayari kukabiliana kijeshi na Korea Kaskazini EUTERS/Lee Jae-Won

Rais Mpya wa Korea Kusini Park Geun-Hye ametoa ahadi ya kuwa tayari kukabiliana kijeshi na jirani zao wa Korea Kaskazini ambao wametangaza nchi hizo mbili zipo kwenye hali ya kivita. Kiongozi huyo mwanamke wa Korea Kusini amesema wamechoshwa na vitisho vya usalama ambavyo vimekuwa vikitolewa na jirani zao wa Korea Kaskazini na hivyo wamejiandaa kwa mapambano.

Matangazo ya kibiashara

Rais Park ametoa onyo hilo kwa Korea Kaskazini baada ya serikali ya Pyongyang kutoa kitisho huenda ikafanya mashambulizi kwa kutumia makombora yake kuilenga nchi hiyo pamoja na kambi za kijeshi za Marekani.

Serikali ya Pyongyang ililazimika kuweka tayari makombora yake kuishambulia Korea Kusini baada ya nchi hiyo kuendelea kufanya mazoezi ya kijeshi wakishirikiana na wanajeshi wa Marekani kitu ambacho Korea Kaskazini wamekiita ni kitisho kwao.

Kiongozi huyo wa Korea Kusini baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi Kim Kwan-Jin pamoja na maofisa wengine wa Kijeshi ndiyo akajitokeza na kusema wapo tayari kukabiliana na Korea Kaskazini ili kulinda wananchi wao.

Park ameweka bayana kwa hali ilivyo sasa wapo tayari kuchukua hatua za haraka za kijeshi na si kidiplomasia tena kutokana na Korea Kaskazini kuonesha dhahiri wanataka kuingia vitani.

Bunge nchini Korea Kaskazini lilipitisha azimio la nchi hiyo kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya jirani zao Korea Kusini kutokana na kukerwa na wao kuwahifadhi wanajeshi wa Marekani na kufanya nao mazoezi.

Rais Park amesema serilali yake inathamini zaidi maisha ya wananchi wake na hivyo hawatakuwa tayari kuona usalama wao unatishiwa na majirani zao wa Korea Kaskazini na ndiyo maana wapo tayari kwa mapambano.

Uhusiano baina ya Korea Kaskazini na Kusini umeingia matatani mara kadhaa kutokana na Pyongyang kutengeza silaha za nyuklia na kuhutiwa na majaribio ya mara kwa mara yanayoidhinishwa na Rais Kim Jong-Un.