KOREA KASKAZINI-KOREA KUSINI-UMOJA WA MATAIFA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban atishwa na hatua zinazochukuliwa na Korea Kaskazini kwa kufungua mtambo wake wa Nyuklia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amekiri kinachoendelea Korea Kaskazini ni hatari
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amekiri kinachoendelea Korea Kaskazini ni hatari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amekiri hali imezidi kuwa ya wasiwasi kwenye eneo la Peninsula na ameionya Serikali ya Korea Kaskazini kuachana na vitosho vyake juu ya utengenezaji wa silaha za nyuklia. Ban amekiri mgogoro uliopo kwa sasa kwenye eneo la Peninsula umekwenda mbali zaidi na ametaka hali ya utulivu irejee na hakuna sababu kwa Serikali ya korea Kaskazini kuingia kwenye mgogoro na Jumuiya ya Kimataifa.

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu Ban ameweka wazi vitisho vya nyuklia siyo mchezo sahihi kwa sasa na badala yake vinaongeza hofu na kukua kwa mgogoro baina ya Korea Kaskazini na majirani zake.

Ban amesema anashawishika kusema huku akiwa na uhakika wa dhati hakuna nchi ambayo ina lengo la kuishambulia Korea Kaskazini eti kwa sababu ya mfumo wake wa kisiasa au sera zao za kimataifa.

Badala yake Katibu Mkuu Ban ameishauri Korea Kaskazini kuachana na harakati zake na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC ili kuhakikisha mgogoro uliopo unasuluhishwa kwa njia ya mazungumzo.

Kauli ya Ban imekuja huku Serikali ya Korea Kaskazini inayoongozwa na Kim Jong-Un ikisema itafungua upya kutumia mtambo wake wa kuzalisha nyuklia walioufungwa mwaka 2007 huku pia wakisema huenda wakaanza kuutumia kurutubisha uranium na kutengeza silaha za nyuklia.

Serikali ya Pyongyang imetangaza mpango wake wa kufungua upya mtambo wake wa kuzalisha nyuklia kipindi hiki ambacho uhusiano wao na majirani zao wa Korea Kusini ukiendelea kudorora.

Kitengo cha Nguvu za Nyuklia nchini Korea Kaskazini ndiyo zimetoa tangazo hilo na kusema wameona kuna umuhimu wa kuongeza mkakati wake wa uzalishaji wa silaha za nyuklia ili kujiimarisha kijeshi dhidi ya maadui zao.

Mtambo huo wa kuzalisha nyuklia upo katika eneo la Yongbyon ambapo kulikuwa kunatumika kuzalisha umeme kwa megawati tano pamoja na kuendesha mpango wa kurutubisha uranium.

Kitengo cha Nguvu za Nyuklia kimesema licha ya kuwa na mkakati wa kuanza kurutubisha madini ya uranium lakini pia watatumia mtambo huo kwa ajili ya kuzalisha umeme kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na upungufu wa umeme.

Mtambo huo wa kuzalisha nyuklia unatajwa utasaidia pia maendeleo ya kijeshi katika nchi hiyo inayoendelea kujijenga kijeshi kila kukicha hatua ambayo imekuwa ikiangaliwa kwa jicho tofauti na majirani zake huko katika eneo la Peninsula.

Korea Kaskazini imefungua mtambo huu na kuonekana ni kama jibu la vitendo vya jirani zao wa Korea Kusini ambao kupitia Rais wao Park Geun-Hye ilitangaza haitishwi kwa lolote kutoka kwa jirani zao ambao wametangaza wapo vitani.