MALI-UFARANSA-UMOJA WA ULAYA

Wakufunzi wa Kijeshi kutoka Umoja wa Ulaya EU waanza kutoa mafunzo kwa Wanajeshi wa Mali ili kuwapa mbinu madhubuti

Wanajeshi wa Jeshi la Mali ambao waanza kupata mafunzo kutoka Umoja wa Ulaya EU ili waweze kukabiliana na adui
Wanajeshi wa Jeshi la Mali ambao waanza kupata mafunzo kutoka Umoja wa Ulaya EU ili waweze kukabiliana na adui France24 / capture d'écran

Waatalam wa Masuala ya Kijeshi kutoka Umoja wa Ulaya EU wanaanza kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali kwa kipindi cha miezi kumi na mitano lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kukabiliana na adui.

Matangazo ya kibiashara

Wakufunzi wapatao 150 ndiyo watakuwa na kibarua cha kutoa mafunzo kwa vikosi vinne tofauti vya Wanajeshi wa Mali ambavyo vimeonekana dhaifu na kushindwa kupambana na Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanashikilia eneo la Kaskazini.

Mpango huo unatarajiwa kujumuisha wanajeshi 550 kutoka nchini 22 za Umoja wa Ulaya EU ambao licha ya kutoa mafunzo lakini wataendelea kuwa na jukumu la kushika doria katika maeneo yaliyokuwa ngome za Makundi ya Kiislam.

Ufaransa ndiyo nchi yenye wanajeshi wengi zao ambao ni 207, huku Ujerumani ikiwa na wanajeshi 71, Uhispania imepeleka wanajeshi 54, Uingereza yenyewe imechangia wanajeshi 40, Jamhuri ya Czech inawajeshi 34, Ubelgiji wanajeshi 25 na Poland nayo imetoa wanajeshi 20.

Wanajeshi wa Ufaransa wameendelea kuwa wengi kutokana na Taifa hilo kuwa la kwanza kuingia nchini Mali kulisaidia jeshi la Taifa kwenye vita ya kuyasambaratisha Wapiganaji wa Makundi ya Kiislam yaliyoshikia maeneo ya Kaskazini.

Mafunzo hayo ya Kijeshi yanatarajiwa kufanyika katika Kambi ya Koulikoro iliyopo kilometa 60 kutoka Mji Mkuu wa Mali, Bamako huku Kiongozi wa Kijeshi wa Ufaransa Brigedia Jenerali Francois Lacointre akiiongoza.

Brigedia Jenerali Lacointre amesema mamlaka nchini Mali zinatambua fika umuhimu wa kujengwa upya kwa Jeshi lake na ndiyo maana walitoa ombi la kusaidiwa kujengewa uwezo kwa wanajeshi wake.

Kiongozi huyo wa Vikosi vya Ufaransa nchini Mali amesema watahakikisha wanatekeleza ombi hilo kwa vitendo ili Mali iweze kuwa na wanajeshi mahiri wanaoweza kukabiliana na adui wakati wowote.

Wanajeshi 4,000 wa Ufaransa waliingia nchini Mali kukabiliana na Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanashikilia Miji ya Gao, Kidal na Timbuktu tangu kufanyika mapinduzi yaliyouangusha Utawala wa Rais Amadou Toumani Toure mwezi machi mwaka 2012.