VENEZUELA

Kampeni za Uchaguzi wa Rais nchini Venezuela zaanza huku Wagombea wakiwa na siku 10 za kupita kwenye Majimbo 23

Kampeni za kuwania kurithi nafasi ya aliyekuwa Rais wa Venezuela Kamanda Hugo Chavez zimeanza rasmi huku Chama Tawala kikiahidi kitaendelea mapinduzi ambayo yaliasisiwa na Kiongozi wao aliyepita.

Wagombea wa nafasi ya Urais nchini Venezuela Kaimu Rais Nicolas Maduro (Kushoto) na Kiongozi wa Upinzani Henrique Capriles (Kulia)
Wagombea wa nafasi ya Urais nchini Venezuela Kaimu Rais Nicolas Maduro (Kushoto) na Kiongozi wa Upinzani Henrique Capriles (Kulia) Reuters/Montaje RFI
Matangazo ya kibiashara

Kampeni hizi zilifunguliwa huku maelfu ya wananchi wakijitokeza kushuhudia kile ambacho kilikuwa kinafanywa na wagombea wawili ambao watachuana kwenye kinyang'anyiro cha tarehe 14 April.

Kaimu Rais wa Venezuela Nicolas Maduro alizindua kampeni za Chama Tawala akiwa katika Mji wa Sabaneta uliopo Magharibi kwa Taifa hilo na ambapo ni nyumbani kwa Marehemu Chavez.

Kiongozi wa Upinzani Henrique Capriles akiambatana na wafuasi wake akajikita katika Jimbo la Monagas lililopo Mashariki mwa nchi hiyo na kuzindua kampeni zake kwa kishindo cha hali ya juu.

Maduro amewaambia wafuasi wa Chama Tawala ya kwamba yeye ni mzalendo ambaye wanamfahamu tangu alipokuwa dereva wa mabasi ya umma ambayo yanatumika kusafirisha abiria.

Kaimu Rais Maduro ametumia muda wake mwingi kwenye uzinduzi wake wa kampeni kurejerea yale ambayo alikuwa ameyaahidi Kamanda Chavez kwa wananchi na amesema wao watahakikisha wanayaendeleza.

Capriles ambaye ni Gavana wa Jimbo la Miranda amesema yeye yupo tayari kuhakikisha anaifanya nchi hiyo kuwa ya kipekee na kupiga hatua za haraka lakini akawataka wananchi kumuunga mkono kwa kumchagua.

Kiongozi huyo wa Upinzani ambaye aliangukwa kwenye uchaguzi wa mwezi Oktoba alipopambana na Marehemu Kamanda Chavez amesema matumaini yake ameyaelekeza kwa wananchi ambao watafanya maamuzi ya kijasiri.

Wagombea wote wamejiambiza kufanya kampeni katika Majimbo yote 23 katika kipindi cha siku kumi zilizotengwa kwa ajili ya kampeni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika tarehe 14 April.

Katika hatua nyingine Rais wa Tume Huru ya Uchaguzi Tibisay Lucena amekanusha vikali madai yaliyotolewa na Upinzani ya kwamba imekuwa ikipendelea Chama Tawala hasa kipindi cha kampeni.

Lucena amesema wagombea wote wawili watapewa uzito sawa kuanzia kipindi cha kampeni na pia wataendesha uchaguzi huo kwa uhuru wa haki ili atakayeshinda aweze kushinda kwa haki na kusiwe na malalamiko.