KOREA KASKAZINI-KOREA KUSINI-MAREKANI

Korea Kaskazini yawazuia wafanyakazi raia wa Korea Kusini kuingia kwenye Ukanda wa Viwanda unaomilikiwa kwa pamoja na pande hizo

Kizuizi kilichowekwa kuingia kwenye Ukanda nchini Korea Kaskazini kimewafanya wafanyakazi kutoka Korea Kusini kukwama nje
Kizuizi kilichowekwa kuingia kwenye Ukanda nchini Korea Kaskazini kimewafanya wafanyakazi kutoka Korea Kusini kukwama nje

Korea Kaskazini imewazuia wafanyakazi raia wa Korea Kusini kuweza kuingia kwenye Ukanda wa Viwanda ambao unamilikiwa kwa pamoja na pande hizo mbili mapema jumatano hatua inayoongeza hofu ya mataifa hayo kuingia kwenye vita. Kampuni ambayo imeshuhudia wafanyakazi raia wa Korea Kusini wakizuiliwa kuingia kuendelea na kazi ipo katika Mji wa Kaesong ambayo imekuwa ikizalisha bidhaa nyingi ambazo zinategemewa na wananchi wa pande zote.

Matangazo ya kibiashara

Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 2004 na kuwa moja ya vitu ambavyo vinawaunganishwa raia wa pande hizo mbili lakini kufungiwa nje kwa wafanyakazi hao kunazua maswali juu ya hatima ya baadaye ya mataifa hayo.

Jumla ya wafanyakazi zaidi ya mia nane kutoka Korea Kusini wanafanyakazi katika katika kampuni hiyo lakini wamejikuta wakifungiwa nje ya lango kuu na kushindwa kuingia kuendelea na kazi zao za kila siku.

Kuzuiliwa kwa wafanyakazi hao wa Korea Kusini nje ya eneo hilo la ukanda wa viwanda huko Korea Kaskazini kumeendelea kuonesha uhusiano baina ya pande hizo mbili umezidi kuzorota na kunahatari mataifa hayo yakaingia vitani.

Korea Kaskazini imeanza kuchukua hatua hizo baada ya kuchoshwa na tabia ya jirani zao Korea Kusini kufanya mazoezi ya kijeshi na Marekani ambao wamekuwa mstari wa mbele kuishinikiza nchi hiyo kuacha kutengeneza silaha za kinyuklia.

Haya yanakuja huku Korea Kusini kupitia Wizara yake ya Ulinzi ikiendelea kusema ipo tayari kuwalinda wananchi wake kwa vitisho vya Korea Kaskazini na hasa wafanyakazi waliopo huko Pyongyang.

Marekani kupitia Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry imesema itakuwa tayari kuwalinda washirika wake kwenye eneo la Peninsula ambao ni Korea Kusini na Japan dhidi ya vitisho vya Korea Kaskazini.

Kauli ya Kerry imeungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini Yun Byung-Se ambaye anasema Marekani inapaswa kushirikiana nao ili kuweza kukabiliana na Pyongyang.

Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon alitoa onyo kwa Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa kufungua kinu cha nyuklia kilichokuwa kimefungwa tangu mwaka 2007.