JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-UMOJA WA MATAIFA

Umoja wa Mataifa UN na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wasaini mkataba wa kukabiliana na vitendo vya ubakaji

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa UN Anayeshughulikia vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia Zainab Hawa Bangura
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa UN Anayeshughulikia vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia Zainab Hawa Bangura

Umoja wa Mataifa UN na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokarsia ya Congo DRC wamesaini mkataba wenye lengo la kukabiliana na vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na Makundi yenye silaha Mashariki mwa Taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Mkataba huo umesainiwa na Waziri Mkuu wa DRC Augustin Matata Ponyo kwa niaba ya serikali ya Kinshasa huku Umoja wa Mataifa UN ukiwakilishwa na Mjumbe Maalum anayeshughulikia Masuala ya Ubakaji na Udhalilishaji wa Kijinsia Zainab Hawa Bangura.

Kusainiwa kwa mkataba huu ni moja ya hatua ambazo zimeendelea kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa UN katika kuhakikisha vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia vinatokomezwa Mashariki mwa DRC.

Mkataba huu ni matokeo ya ziara ya Mjumbe wa UN Bangura ambaye ameweza kuzuru maeneo ambayo yamekuwa yakitajwa kuathiriwa zaidi na vitendo vya ubakaji vinavyochochewa na uwepo wa vita.

Punde baada ya kusainiwa kwa mkataba huo Serikali ya Kinshasa imejiapiza kuhakikisha unafanya kazi katika kuhakikisha inawaokoa wanawake na vitendo hivyo vinavyofanywa na wanaume wenye silaha.

Mkataba huu unasaini siku kadhaa baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC kupitisha azimio la kupeleka Kikosi Maalum Mashariki mwa DRC kikiwa na jukumu la kukabiliana na Makundi yanayomiliki silaha na si kulinda amani kama ilivyozoeleka.

Juma lililopita wakati Mjumbe wa UN Bangura akiwa kwenye ziara yake na kuambatana na Waziri Jinsia Watoto na Jamaa Genevieve Inagosi alikiri kuwa vitendo vya ubakaji vimekuwa vikiota mizizi kwenye maeneo yenye vita.

Bangura akiwa nchini DRC alifanikiwa kukutana na Rais Joseph Kabila, Makundi ya Wanawake na kutembelea Hospitali ambazo zimekuwa zikiwahudumia wanawake wanaobakwa katika Majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Umoja wa Mataifa UN ulitoa ripoti baada ya kufanya uchunguzi wake na kusema licha ya Makundi ya watu wenye silaha kufanya ubakaji lakini wanajeshi wa Jeshi la Serikali FARDC nalo linahusika kwenye vitendo hivyo.