MAREKANI

Rais Barack Obama aendelea kuongeza shinikizo kwa Baraza la Seneti lipitishe Sheria ya Mabadiliko ya Umiliki wa Silaha

Rais wa Marekani Barack Obama akiwahutubia wananchi wa Taifa hilo huko Miami
Rais wa Marekani Barack Obama akiwahutubia wananchi wa Taifa hilo huko Miami REUTERS/Jonathan Ernst

Rais wa Marekani Barack Obama ameendelea kulishinikiza Baraza la Seneti nchini mwake kuhakikisha linapitisha mabadiliko ya sheria ya umiliki wa silaha ambayo yatasaidi kukabiliana na vitendo vya kihalifu.

Matangazo ya kibiashara

Obama amesema huu ni wakati kwa Baraza la Seneti kuangalia sheria iliyopo sasa na mapungufu yake ambayo yamechangia wananchi wengi kupoteza maisha baada ya kushuhudia watu wenye silaha wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara.

Kiongozi huyo wa Marekani amelikumbusha Baraza la Seneti ya kwamba wananchi wengi wamekuwa wakiunga mkono kufanyika kwa mabadiliko ya sheria hiyo ya umiliki wa silaha kutokana na kuona madhara yake katika jamii.

Obama pia akawageukia Wanaharakati ambao wamekuwa wakiongoza kampeni mbalimbali za kutaka serikali kuachana na mkakati wake wa kufanya mabadiliko ya sheria ya umiliki wa silaha na kusema hawana nia njema na wananchi ambao wanaathiriwa na mashambulizi.

Rais Obama akihutubia mamia ya wananchi amesema matukio ya hivi karibuni ambayo yamechangia hivyo huko Colorado na Connecticut ni ushahidi wa kutosha kabisa ya kwamba Baraza la Seneti linapaswa kufanya mabadiliko ya sheria hiyo.

Kiranja huyo wa Dunia amesema yeye haamini kama watu wanapaswa kumiliki silaha ili kuwa kitisho cha usalama kwa wengine na badala yake silaha hizo zinafaa kutumika kwenye maeneo yenye vita.

Baraza la Seneti linatarajiwa kukutana juma lijalo kupitia sheria hiyo huku kukiwa na dalili huenda wakapitisha mabadiliko ya sheria hiyo na kuweka masharti magumu kwa wale wanaomiliki aua wanataka kumiliki silaha.

Miongoni mwa matukio ambayo yameishawishi serikali ya Rais Obama kuona kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ya sheria ya umiliki wa silaha ni pamoja na kushambuliwa kwa watu wakiwa kwenye ukimbu wa sinema huko Colorado na kusababisha vifo vya watu 12.

Shambulizi jingine ambalo bado lipo kwenye kumbukumbu za wananchi wengi wa Marekani wakiwa ni pamoja na wazazi ni vifo vya watoto wa shule 20 waliouawa huko Connecticut baada ya mtu mwenye silaha kuwashambulia.

Jimbo la Connecticut linatarajiwa kuidhinisha sheria ya kudhibiti umiliki wa silaha siku ya jumatatu ili kuepukana na mauaji zaidi ambayo yamekuwa yakitekelezwa na watu wenye silaha katika eneo hilo.