ARGENTINA

Watu 56 wapoteza maisha nchini Argentina kufuatia kutokea kwa mafuriko mabaya yaliyochangiwa na kunyesha kwa mvua

Kikosi cha Uokoaji nchini Argentina kikiwasaidia watu ambao wameathiriwa na mafuriko yaliyopiga nchi hiyo
Kikosi cha Uokoaji nchini Argentina kikiwasaidia watu ambao wameathiriwa na mafuriko yaliyopiga nchi hiyo

Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye mafuriko mabaya kuikumba nchi ya Argentina imefikia 56 kitu kilichoifanya serikali kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa huku Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis akituma salamu zake za pole.

Matangazo ya kibiashara

Takwimu zinaonesha watu wanaotajwa kufika 48 wamepoteza maisha katika eneo la La Plata lililopo kilometa 60 Kusini mwa Mji Mkuu huku watu sita wakifikwa na mauati katika eneo la Buenos Aires na wengi wawili kwenye miji mingine.

Mafuriko hayo ni matokeo ya mvua iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo katika Jimbo la Buenos Aires na La Plata na kuchangia uwepo wa maji mengine yaliyosababisha hasara kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.

Waathirika wengi wameanza kuonekana siku ya pili baada ya mvua hiyo kupunguza makali yake na ndipo Mamlaka zenye jukumu la uokoaji zikaanza kufika maeneo hayo kwa ajili ya kutoa msaada.

Miili ya wale waliofikwa na mauti imeanza kuopolewa kwenye maji zoezi ambalo linatajwa kukabiliwa na vikwazo kadhaa kutokana na miundombinu kuharibiwa na mvua hivyo na hivyo kikosi cha uokoaji kushindwa kufika kwa wakati.

Gavana wa Jimbo la Buenos Aires Daniel Scioli amesema kwa sasa miili mingi imeanza kuonekana juu ikiwa imezagaa kutokana na kiwango cha maji kuanza kupungua kwenye Jimbo lake.

Gavana Scioli amesema kuna uwezekano mkubwa idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na nyumba nyingi kuathirika na mafuriko hayo huku watu wengi wakiwa hawajulikani walipo baada ya mvua hizo za siku mbili.

Afisa wa Jiji Santiago Martorelli amejitokeza kwenye Televisheni ya Taifa na kusema mafuriko hayo ni janga na hivyo wamelazimika kufungua ofisi zote za serikali pamoja nashule katika kipindi hiki kigumu.

Martorelli amesema kuna mamia ya watu ambao wamejihifadhi kwenye mapaa ya manyumba pamoja na kwenye miti wakisubiri kuokolewa na hivyo wanajeshi na polisi wamejumuishwa kwenye kikosi cha uokoaji.

Mafuriko haya ndiyo yanatajwa kuwa mabaya zaidi kutoka nchiniArgentina katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na tayari Rais Cristina Kirchner aliyezuru ghafla eneo la La Plata amesema watachukua hatua za dharura kuwasaidia waathirika.