KOREA KASKAZINI-KOREA KUSINI-MAREKANI

Hofu ya kuibuka vita kati ya Korea Kaskazini na Marekani yaongezeka huku kila upande ukiweka sawa zana zake za Kijeshi

Wanajeshi wa Marekani na Korea Kusini wakiendelea na mazoezi kujiwinda na mashambulizi kutoka Korea Kaskazini
Wanajeshi wa Marekani na Korea Kusini wakiendelea na mazoezi kujiwinda na mashambulizi kutoka Korea Kaskazini

Hofu ya kuibuka kwa vita vya tatu vya dunia imeendelea kukua baada ya Korea Kaskazini na Marekani kuendelea kutunishiana misuli kutokana na kila upande kuweka tayari silaha zake kwa ajili ya kujibu mashambulizi.

Matangazo ya kibiashara

Korea Kaskazini imelazimika kupeleka makombora yake katika Pwani yake ya Mashariki kukabiliana na zana za kijeshi za Marekani ambazo zimepelekwa katika Kambi yake ya Guam na kuongeza hofu ya kuzuka vita.

Hatua ya Korea Kaskazini kupeleka makombora yake katika Pwani ya Mashariki imeifanya Korea Kusini kushikwa na hofu huenda ikajikuta unashambuliwa wakato wowote kutokana sasa na majirani zao.

Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini Kim Kwan-Jin amesema umbali ulitumika kuweka makombora ya Korea Kaskazini unaonesha kila dalili ya kwamba nchi hiyo imedhamiria kufanya mashambulizi.

Kwan-Jin amesema nchi yake haiwezi kuendelea kuvumilia vitisho na uchokozi ambao unafanywa na Korea Kaskazini dhidi yao na hivyo nao watakuwa tayari kukabiliana nao pindi watakapowashambulia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon kwa upande wake ameiangukia Korea Kaskazini na kuitaka kuachana na mpango wake wa kutaka kuishambulia Korea Kusini na Marekani.

Ban amesema kile kinachofanywa na Pyongyang si kitu cha kuungwa mkono kwani kinaweza kikachangia kuzuka kwa vita na kuleta madhara makubwa kwa wananchi wa mataifa hayo na dunia kwa ujumla.

Marekani yenyewe inaonekana kutojali vitisho na uchokozi wa Korea Kaskazini na kusema wao wapo tayari na ndiyo maana wameimarisha ulinzi katika Kambi yao ya Guam kukabiliana na mashambulizi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Victoria Nuland amesema wamejiimarisha kiulinzi na kuweka vifaa maalum kujikinga na makombora ya Korea Kaskazini huko Guam.

Korea Kaskazini imelazimika kuchukua hatua hiyo ya kutaka kuzishambulia Marekani na Korea Kusini kutokana na kuchukizwa na kitendo cha mataifa hayo kufanya mazoezi ya kijeshi.