IRAN-KAZAKHSTAN

Mazungumzo ya kusaka suluhu ya mgogoro wa nyuklia unaoikabili Iran yameanza na kuzileta pamoja pande sita

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad akikagua kinu kimoja wapo cha nyuklia kinachomikiliwa na taifa hilo
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad akikagua kinu kimoja wapo cha nyuklia kinachomikiliwa na taifa hilo

Iran na Mataifa yenye nguvu Duniani kwa pamoja wameanza mazungumzo ya kujadili mgogoro wa nyuklia wa Tehran ambao nchi hiyo unataka ukubaliwe kutokana na lengo lake ni kuwasaidia wananchi wake kupata nishati ya kudumu. Mazungumzo hayo yameanza kufanyika nchini Kazakhstan na kuzileta pamoja pande sita zikiwa ni nchini wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC.

Matangazo ya kibiashara

Mataifa hayo sita yatakuwa na mazungumzo ya siku mbili ikiwa ni mkakati wa kutaka kuishawishi Iran kuachana na mapngo wake wa kurutubisha nyuklia inayotajwa kuwa na madhara makubwa kwa binadamu.

Mataifa hayo wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ndiyo walihusika pakubwa katika mkakati wa kuiwekea vikwazo Iran ambayo kwa sasa inapitia kwenye wakati mgumu kiuchumi.

Serikali ya Iran kwenye mazungumzo hayo inawakilishwa na Mkuu wa Upatanishi Saeed Jalili ambaye kabla ya kuanza mkutano huo amesema msimamo wao utasalia kama awali na kuyataka mataifa hayo kuheshimu uamuzi wao.

Jalili amesema wamekuwa wakirutubisha uranium kwa ajili ya manufaa ya wananchi wao waweze kupata nishati ya umeme kwa uhakika na kulipia gharama kidogo tofauti na ilivyo kwa sasa.

Mpatanishi Mkuu huyo wa Iran amekanusha madai yanayoelekezwa kwa nchi yake ya kwamba imekuwa ikirutubisha madini ya uranium wakiwa na lengo la kutengeneza silaha za nyuklia.

Iran imekuwa katika mgogoro na jirani zao wa Israeli wanaokerwa na hatua ya Serikali ya Tehran kumiliki nyuklia wakiamini inajiandaa ili kuishambulia nchi hiyo kijeshi kwa kutumia zana hizo.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu mapema juma hili amenukuliwa akisema hawatokuwa tayari kuona mazungumzo haya ya pande sita hayatoi suluhu la kudumu katika kuidhibiti Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya EU Catherine Ashton kabla ya kuanza kwa mkutano huo aliwaambia wanahabari anaelekea kwenye kikao hicho na kutaka mapendekezo ya Jumuiya ya Kimataifa yaheshimiwe na Iran.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amenukuliwa akisema ni Iran yenyewe itakayofanya maamuzi juu ya mpango wake na kama inataka kumiliki nyuklia lazima ifuate njia salama.