JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Muungano wa Seleka umeanza mchakato wa kuunda Jeshi la Taifa lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama

Wapiganaji wa Muungano wa Seleka watakaokuwa sehemu ya Jeshi la Taifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wapiganaji wa Muungano wa Seleka watakaokuwa sehemu ya Jeshi la Taifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati REUTERS/Alain Amontchi

Muungano wa Seleka ambao umefanya mapinduzi ya serikali nchini jamhuri ya Afrika ya kati umeanza mchakato wa kuajiri vijana ambao wataunda Jeshi la Taifa ikiwa ni sehemu ya kusimamia usalama.

Matangazo ya kibiashara

Mungano wa Seleka unaoongozwa na Michel Djotodia aliyejitangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati majuma karibu mawili umelazimika kuchukua hatua hiyo ukiwa na lengo la kutaka kuwaunganisha wapiganaji wao wote.

Seleka kupitia Koplo Valentin William Saba anayesimamai mchakato huo amesema watahakikisha wanapata vijana mahiri watakaojumuishwa kwenye Jeshi la Taifa litakalokuwa na jukumu la kulinda nchi.

Koplo Saba amesema watatoa mafunzo ya kutosha kwa wanajeshi hao wote ambao wataunda Jeshi la Taifa na wanaamini hiyo itakuwa ni hatua moja ya kuhakikisha utulivu katika Taifa hilo unapatikana.

Mpango huo unakuja kipiondi hiki ambacho duru za kiusalama ndani ya Serikali ya Seleka zikieleza tayari wameanza mkakati wa kuyanyang'anya silaha makundi yote yanayomiliki zana hizo.

Taarifa hiyo inasema hata mkakati wa kuwaajiri wanajeshi wapya ni sehemu ya kuhakikisha silaha zinazomilikiwa na watu binafsi aua makundi zinarejea kwenye mikono ya serikali ili kuondoa uhalifu.

Naye Kanali Omar Bourdas ambaye ni mmoja wa maofisa wa Muungano wa Seleka amesema kinachofanyika si kutavunja makundi ambayo yapo bali wanafanya hivyo ili kuwa na jeshi litakaloweza kukabiliana na adui.

Kanali Bourdas amesema wao watakuwa tofauti na Utawala wa Rais Francois Bozize ulioshindwa kuyaleta pamoja makundi nchini humo na kuchangia kuwepo kwa uasi kila kukicha.

Hadi sasa watu mia tatu wamejiandikisha wakitaka kujumuishwa kwenye Jeshi la Taifa wakiwemo wanaume na wanawake na mchakato wa kusaka wale wanaofaa kujumuishwa umeshaanza.