DRCONGO-M23

Wananchi wa Nyiragongo wayatoroka makwao kukimbia wito wa maandamano ulioitishwa na waaasi wa M23

Wanajeshi wa MONUSCO katika doria
Wanajeshi wa MONUSCO katika doria

Wananchi kadhaa wengi wao wakiwa vijana, wameyatoroka makwao mapema leo asubuhi katika tarafa ya Nyiragongo Mkoa wa Kivu ya kaskazini na kukimbilia katika miji ya Kabanga na Kabuhanga mpakani mwa DRCongo na Rwanda. Duru kutoka katika eneo hilo zaarifu kuwa wananchi hao wamepinga wito uliotolewa na waasi wa kundi la M23 wa kuandamana hii leo kutoka Kibumba hadi Goma, kupinga ujio wa kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kitacho kabiliana na makundi ya waasi.

Matangazo ya kibiashara

Duru sahihi kutoka katika eneo hilo zaarifu kuwa kundi la M23 limeahirisha maamdamano hayo baada ya tukio hilo, na huenda wakapanga maandamano mengine siku ya jumapili juma hili.

Kwa mujibu wa msemaji wa mashirika ya kiraia katika eneo hilo, Omar Kavota, amesema Wananchi wakaazi wa tarafa ya Nyiragongo hawakupenda kusihiriki katika maandamano na kuhofia uslama wao na ndio maana wameamuwa kuyatoroka makwao na kukimbilia katika maeneo ya mpaka, wakihofia ulipizaji kisase wa kanali Makenga na watu wake.

Msemaji huyo wa mashirika ya kiraia, ameitolea wito jamii ya kimataifa kuingilia kati na kuwalinda raia kuhusu vitisho vya kundi hilo la M23 ambalo linaendesha kampeni kwa wananchi ya kupinga ujio wa kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa katika eneo hilo.

Hapo jana mashirika ya kiraia yalilituhumu kundi la waasi wa M23 kueneza kampeni ya chuki dhidi ya kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kitachokuwa na lengo la kuyasambaratisha makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Omar Kavota alitaja matukio kadhaa ya mikutano ya hadhara inayoendeshwa na kundi hilo katika maeneo inayo yakalia na kuwataka wananchi kupinga ujio wa kikosi cha Umoja wa mataifa nchini humo.

Kundi la M23 linapinga vikali hatuwa ya Umoja wa Mataifa ya kutuma kikosi hicho nchini DRCongo, ambapo mwenyekiti wa kisiasa wa kundi hilo la waasi Bertrand Bisimwa amesema kuunda kikosi hicho Umoja wa Mataifa umechagua njia ya vita.

Serikali ya DRCongo kupitia waziri wake wa mambo ya nje Raymond Tshibanda amewataka waasi wa kundi la M23 kulifuta kundi hilo ili kuepuka mapambano na kikosi hicho maalum cha Umoja wa Mataifa.