MALI-MAURITANIA

Raia wa Mali wakabiliwa na hali tete katika kambi za wakimbizi

Olivier Epron/Wikimedia Commons

Maelfu ya raia toka toka nchini Mali wanaishi katika mazingira magumu katika kambi za wakimbizi nchini Mauritania. Ripoti ya Madaktari wasiokuwa na mipaka MSF imethibitisha uwepo wa hali hiyo na kubainisha kuwa takribani watoto wawili hufariki kila siku kutokana na hali mbaya ya maisha.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti hiyo imeeleza kuwa wastani wa watu 3000 wanatumia choo kimoja na hali mbaya zaidi imeshuhudiwa baada ya kuongezeka kwa wakimbizi wengine waliowasili mwezi januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa UN, zaidi ya watu 270,000 wamepotea makwao na wengine zaidi ya 170,000 wamekimbilia nchi jirani za Burkina Faso, Mauritania na Niger tangu kuzuka kwa machafuko ya nchini Mali mwanzoni mwa mwaka jana.

Majeshi ya Ufaransa yakishirikiana na vikosi vya Mali waliendesha mashambulizi katika eneo la kaskazini mwa Mali kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu na kuwatimua wapiganaji wa kiislamu katika ngome zao muhimu kaskazini mwa nchi ya Mali.

Hata hivyo bado haijatengamaa nchini humo kwani kumeendelea kushuhudiwa mashambulizi ya kujitoa muhanga mara kadhaa yanayotekelezwa na wapiganaji hao wa kiislamu.