KOREA KASKAZINI-MAREKANI-KOREA KUSINI

Obama ashauri Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa kuanzisha vita

Reed / Reuters

Rais wa Marekani Barack Hussein Obama hatimaye amefungua kinywa chake na kuishauri Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa kutaka kuingia kwenye vita katika kipindi hiki wakati kukiwa na uvumi kuwa serikali ya Pyongyang inataka kushambulia Washington kwa makombora.

Matangazo ya kibiashara

Obama ametoa kauli hiyo akiwa katika Ikulu yake maarufu kwa jina la White House na kueleza hakuna mtu yeyote ambaye anapenda kushuhudia Dunia inaingia kwenye mgogoro utakaochangia vita.

Aidha Rais Obama amesisitiza umuhimu wa serikali ya Korea Kaskazini kuheshimu sheria na taratibu kama inavyofanyika kwa nchi nyingine duniani ili kuepusha migogoro zaidi.

Korea Kaskazini pia haikukwepa kidole cha lawama kutoka kwa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi tajiri zaidi duniani maarufu kama G8 walipokutana nchini Uingereza.

Akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague amesema endapo Pyongyang itafanya jaribio jingine la nyuklia hawatasita kuchukua hatua kali dhidi yake ikiwemo vikwazo vipya ambavyo vitaafikiwa katika baraza la usalama la umoja wa mataifa UNSC.

Hofu ya kutekelezwa kwa mashambulizi kutoka Korea Kaskazini kulenga Marekani na rafiki zake Japan na Korea Kusini imeendelea kuchanja mbuga licha ya makaripio mbalimbali kuzidi kutolewa kila uchao.