IRAN

Tetemeko kubwa la ardhi latetemesha Iran, zaidi ya watu 40 wauawa

Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa richa 7 nukta 8 limetokea Kusini Mashariki mwa Iran na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40.

Matangazo ya kibiashara

Maafisa wa usalama wanasema kuwa wanahofia kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka baada ya tetemeko hilo kutikisa karibu na mpaka wa Pakistan na kusikika hadi Abu Dhabi na New Delhi nchini India.

Watu watano wamethibitishwa kuuawa katika mpaka wa Pakistan huku ofisa wa serikali ya Tehran akisema huenda idadi ya watu waliopoteza maisha ikaongezeka.

Walioshuhudia tetemeko hilo la ardhi wameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa tetemeko hilo lilitokea wakati watu walipokuwa ndani ya nyumbani zao na lilisikika kwa muda mrefu.

Watu waliokuwa ndani ya Majengo marefu mjini Karachi, New Delhi na Dubai walilazimishwa kuondoka ndani ya majengo hayo kwa hofu kuwa huenda tetemeko hilo lingeangusha majengo hayo.

Wiki iliyopita, tetemeko la ardhi lenye richa 6 nukta 3 ilitokea nchini humo na kusababisha vifo vya watu 37 na kuwajeruhi zaidi ya 800 Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.

Tetemo lingine kubwa nchini humo lilitokea mwaka 2003 na kusababisha watu 31,000 kupoteza maisha yao na kuharibu majengo ya Kihistoria mjini Tehran.

Wataalam wa maswala ya matetemeko ya ardhi wanasema kuwa hili ndilo tetemeko kubwa na baya zaidi kuwahi kuikumba Iran ndani ya miaka 40.

Wakati mkasa huo ukitokea, rais wa Iran Mahmud Amhaminenad amekuwa akiendelea na ziara yake katika mataifa ya Magharibi ya Afrika.