UINGEREZA

Maelfu watoa heshima za mwisho kwa Margaret Thatcher

Mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Margaret Thatcher yamefanyika siku ya Jumatano jijini London nchini Uingereza na kuhudhuriwa na maelfu ya watu wakiwemo viongozi mashuhuri.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi mbalimbali duniani walihudhuria ibada ya wafu ya Thatcher katika Kanisa la Mtakatifu Paulo, na kuhudhuriwa pia na Malkia Elizabeth wa pili na Mume wake Prince Philip.

Miongoni mwa wageni wengine mashuhuri waliofika katika ibada hiyo ni pamoja na aliyekuwa wakati mmoja Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Henry Kissinger na Makamu wa rais wa zamani Dick Cheney.

Mbali na viongozi hao, ibada hiyo pia ilihudhuriwa pia na Mawaziri 32 wa serikali ya Waziri Mkuu wa sasa David Cameron na Mawaziri 30 waliohudumu wakati wa utawala wa Thatcher na kufanyika kwa njia ya amani.

Usalama uliimarishwa katika mitaa ya London huku maelfu wakijitokeza kuhudhuria na kushuhudia msafara uliongozwa na jeshi.

Waziri huyo Mkuu wa zamani aliongoza Uingereza kati ya mwaka 1979 hadi 1990 na alifariki dunia tarehe 8 mwezi huu akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kupata kiharusi.

Thatcher ameapewa mazishi kama ya kitaifa yakiongozwa na jeshi kuonesha heshima na mchango mkubwa aliotoa  kwa nchi ya Uingereza wakati wa uongozi wake.

Waziri Mkuu huyo wa zamani atakumbukwa sana katika juhudi zake za kutetea sera za Uingereza na kuongoza vita dhidi ya Argentina na ukakamavu wake.