UINGEREZA

Margaret Thatcher kuzikwa leo usalama waimarishwa jijini London

Usalama umeimarishwa katika mitaa ya jijini London nchini Uingereza huku maelfu wakijitokeza kuhudhuria na kushuhudia mazishi za Waziri Mkuu wa zamani Margaret Thatcher.

Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya polisi elfu nne wanaimarisha usalama huku zaidi ya wageni waalikwa zaidi ya elfu mbili kutoka kote duniani wakihudhuria mazishi hayo katika Kanisa la Mtakatifu Paulo.

Maafisa wa usalama wa Scotland Yard wamesema wanatarajia maandamano wakati mwili wa Thatcher utakapokuwa unapitishwa katika barabara za jiji la London.

Waziri huyo Mkuu wa zamani aliongoza Uingereza kati ya mwaka 1979 hadi 1990 na alifariki dunia tarehe 8 mwezi huu akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kupata kiharusi.

Thatcher anapewa mazishi kama ya kitaifa yakiongozwa na jeshi kuonesha heshima na mchango mkubwa aliotoa  kwa nchi ya Uingereza wakati wa uongozi wake.

Mazishi ya Thatcher yanahudhuriwa na Malkia, Mawaziri 32 wa serikali ya Waziri Mkuu wa sasa David Cameron na Mawaziri 30 waliohudumu wakati wa utawala wa Thatcher.

Waziri Mkuu huyo wa zamani atakumbukwa sana katika juhudi zake za kutetea sera za Uingereza na kuongoza vita dhidi ya Argentina na ukakamavu wake.