MAREKANI

Moto wasababisha maafa katika kiwanda cha mbolea nchini Marekani

Polisi katika jimbo la Texas nchini Marekani wanasema kuwa kati ya watu watano  na 15 wameuawa baada ya kutokea kwa mlipuko wa moto katika kiwanda cha kutengeneza mbolea katika eneo la Waco.  

Matangazo ya kibiashara

Aidha, polisi wamebainisha kuwa zaidi ya watu 160 wamejeruhiwa katika  mlipuko huo wakiwemo maafisa wa kuzima moto  waliofika katika eneo hilo kuuzima moto huo bila ya  mafanikinio na wengine bado hawajapatikana.

Mlipuko huu unakuja siku mbili baada ya kutokea kwa mashambulizi ya mabomu mjini Boston wakati wa mbio ndefu za Boston Marathon siku ya Jumatatu na kusababisha vifo vya watu watatu.

Moto huo ulitokea Jumatano usiku pia umewaathiri wazima moto kutokana na moto mkubwa katika kiwanda hicho na idadi kubwa ya watu kujeruhiwa kwa kudungwa na vioo na matofali ya jengo hilo.

Hadi sasa maafisa wa uokoaji wanasema kuwa haijafamika chanzo cha kuzuka kwa moto huo wakati huu uchunguzi unapoendelea kubaini kilichotokea.

Duru zinasema kuwa idadi kubwa ya watu bado wamekwama katika jengo hilo wakimemo maafisa wa uokoaji na juhudi zinafanyika kuwaokoa.

Gavana wa jimbo la Texas Rick Perry amesema bado wanafanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa taarifa zozote kuhusu mkasa huo mbaya katika siku za hivi karibuni nchini humo.