SYRIA

Marafiki wa Syria wakutana Istanbul kuzungumza na wapinzani wa Rais Assad

Mataifa yanayounga mkono harakati za upinzani dhidi ya Rais wa Syria Bashar al-Assad yanakutana jumamosi hii huko Instanbul, mataifa hayo 11 yanayotambulika kama marafiki wa Syria yakijumuishwa na Marekani, mataifa ya Ulaya na nchi za kiarabu yatazungumza na viongozi wakuu wa upinzani wa Syria.

Matangazo ya kibiashara

Wapinzani wana ombi la kupatiwa silaha toka kwa mataifa yanayowaunga mkono, lakini mkutano wa hii leo unatarajiwa kuja na jibu endapo mataifa hayo ya magharibi na nchi za kiarabu zitawaunga mkono zaidi hususani katika msaada wa silaha.

Mapema juma hili Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisema wanatarajia mazungumzo hayo yatakuwa na jitihada chanya ili kuhakikisha hawashiriki katika kulidumbukiza taifa hilo mahala pabaya zaidi.

Baadhi ya nchi hususani Urusi zimekuwa zikiwashutumu marafiki wa Syria kutokuwa na nia njema katika upatikanaji wa suluhu ya kudumu itakayomaliza machafuko hayo ya zaidi ya miaka miwili yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya elfu sabini na maelfu kuyakimbia makazi yao.