MAREKANI-BOSTON

Taarifa zaendelea kukusanywa kabla ya kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa wa mauaji ya Boston

REUTERS/Brian Snyder

Polisi na wanainteligensia wa nchini Marekani wanaendelea kukusanya taarifa muhimu kabla ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa mmoja wa mashambulizi ya mabomu katika mbio za Marathon mjini Boston, mtuhumiwa huyo Dzhokhar Tsarnaev alijeruhiwa katika mapambano na askari siku ya ijumaa tukio ambalo lilisababisha kifo cha kaka yake Tamerlan Tsarnaev ambaye naye alihusika katika tukio hilo.

Matangazo ya kibiashara

Mtuhumiwa aliyesalia hai mpaka sasa Dzhokhar Tsarnaev anapatiwa matibabu katika hospitali moja mjini Boston, Madaktari wamesema hali yake inaendelea vizuri ingawa hawezi kuzungumza kutokana na kukabiliwa na majeraha ya risasi katika shingo yake.

Vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akiulizwa maswali na kuyajibu kwa njia ya maandishi ikiwa ni hatua mojawapo ya kuchunguza kiini cha mashambulizi hayo.

Huenda mshtakiwa huyo akakabiliwa na adhabu ya kifo endapo atakutwa na hatia ya kutumia silaha za maangamizi katika kutekeleza mauaji hayo.

Kijana huyo na ndugu yake Tamerlan aliyeuawa siku ya Ijumaa walitekeleza mashambulizi yaliyowajeruhi watu 180 huku wengine watatu wakipoteza maisha.

Tsarnaev na Tamerlan wanatajwa kama wanachama wa kundi moja ya Waislam wenye msimamo mkali lililopo huko Chechnia na tayari taarifa za kijasusi zimeanza kuihusisha Urusi kwenye sakata hili.