NIGERIA

Takribani watu 185 wauawa kwenye mapigano kati ya kundi la Boko Haram na wanajeshi wa Nigeria

news.yahoo.com

Mapigano kati ya wanajeshi wa Nigeria na wapiganaji wa kundi la kiislamu la Boko Haram yamesababisha vifo vya watu takribani 185 katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Mapigano hayo yalizuka siku ya ijumaa katika eneo la Baga na kusababisha baadhi ya raia kuyakimbia makazi yao wengi wao wakielekea katika maeneo yanayozunguka ziwa Chad, shirika la habari la AP limeripoti.

Matangazo ya kibiashara

Maofisa wa serikali ya nchi hiyo wamefika katika eneo lililoathiriwa kujionea uharibifu uliofanyika katika nyumba, maeneo ya biashara, magari na mali nyingine zilizochomwa.

Kiongozi wa serikali katika eneo la Baga Lawan Kole amesema takribani miili ya watu 185 waliouawa imepatikana na kuzikwa siku ya jumapili jioni huku wengi wakishindwa kutambuliwa kutokana na kuungua vibaya na moto uliowashwa katika mji huo.

Kundi la wapiganaji la Boko Haram linataka kuachiwa huru kwa wanachama wake ambao wanashikiliwa na serikali ya Nigeria na pia wanataka nchi hiyo iendeshwe kwa kufuata sheria ya kiislamu ya sharia.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la AP, mashambulizi yanayoendeshwa na Boko Haram tangu mwaka 2009 yamesababisha vifo vya watu takribani 1584 kabla ya mauaji ya siku ya ijumaa.