Marekani yaahidi msaada zaidi wa kijeshi kwa Israel
Imechapishwa:
Serikali ya Marekani imeendelea kujiimarisha kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati kufuatia kutoa msaada wa kijeshi kwa jeshi la Israeli kutokana na kile ilichodai usalama wao na maswahiba zao hao upo hatarini kwa kuwa Irani inamiliki silaha za kinyuklia. Msaada huo wa zana za kijeshi imetangazwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ambaye amekamilisha ziara yake nchini Israeli.
Katika ziara hiyo Marekani kupitia kwa Waziri Hagel imeahidi kuendelea kuiunga mkono Israeli katika kuimarisha usalama wao ambao upo hatarini kutokana na silaha za nyuklia zinazomilikiwa na Irani.
Akiwa nchini humo Hagel amekutana na Waziri wa Ulinzi wa Taifa hilo Moshe Yaalon na kuhitimisha ziara yake kwa kuzungumza na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Netanyahu amesema uhusiano baina yao na Marekani unahatarishwa na vitisho vya Irani ambayo imekuwa ikisambaza silaha nzito kwa makundi ya wapiganaji wenye misimamo mikali.
Akiongea na waandishi wa habari nchini humo, Hagel amebainisha kuwa mpango wao sio wa kutaka kuipinga Irani bali ni kuhakikisha wanajilinda dhidi ya mapambano kutoka kwa maadui zao wanaotaka kuwashambulia.