MAREKANI-BOSTON

Mtuhumiwa wa mauaji ya Boston afunguliwa mashtaka ya kumiliki silaha za maangamizi

REUTERS/Jim Bourg

Waendesha Mashtaka nchini Marekani katika Mji wa Boston wamemfungulia mashtaka ya kumiliki silaha za maangamizi mtuhumiwa wa shambulizi la bomu lilisababisha vifo vya watu watatu Dzhokhar Tsarnaev ambaye anaendelea kupatiwa matibabu. Msemaji wa Ikulu Jay Carney amesema mtuhumiwa huyo hatoshtakiwa kwenye Mahakama za Kijeshi.

Matangazo ya kibiashara

Ikulu ya Marekani ililazimika kutoa ufafanuzi wa kina baada ya kuwepo kwa shinikizo la kutaka kijana huyo ashtakiwe kwenye mahakama za kijeshi.

Kwa mujibu wa madaktari mtuhumiwa huyo alijeruhiwa vibaya kwenye koo na huenda asiongee tena, na iwapo atakutwa na hatia ya kutumia silaha hizo za maangamizi atakabiliwa na adhabu ya kifo.

Taarifa toka nchini humo zilidokeza kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akiulizwa maswali na kuyajibu kwa njia ya maandishi ikiwa ni hatua mojawapo ya kuchunguza kiini cha mashambulizi hayo.

Wachunguzi toka shirika la ujasusi la Marekani FBI bado wanamatumaini huenda wakapata taarifa muhimu toka kwa Tsarnaev ili kujua kama kuna mashambulizi mengine yalipangwa kutekelezwa.

Dzohkhar Tsarnev na kaka yake Tamrelan Tsarnev aliyeuawa siku ya ijumaa walitekeleza mashambulizi ya mabomu yaliyowajeruhi watu 200 na huku wengine watatu wakipoteza maisha.