Bangladeshi

Takriban Watu 82 wapoteza maisha katika Ajali ya kuporomoka kwa Orofa nchini Bangladesh

Raia wakijaribu kuoakoa Wapendwa wao kutoka katika vifusi vya Jengo lililoporomoka nchini Bagladesh
Raia wakijaribu kuoakoa Wapendwa wao kutoka katika vifusi vya Jengo lililoporomoka nchini Bagladesh Reuters

Takriban watu 82 wamepoteza maisha baada ya Jengo la Orofa nane lililokuwa na viwanda kadhaa vya nguo na maelfu ya Wafanyakazi kuanguka nchini Bangladesh, huku watu wengine zaidi wakihofiwa kupoteza maisha.

Matangazo ya kibiashara

Mamia ya wanakikosi wa uokoaji na Jeshi wanashirikiana kuwatafuta manusura wa ajali hiyo huku miili ya Watu waliopoteza maisha na majeruhi wamekuwa wakiondolewa katika eneo la ajali, na kuelezwa kuwa zoezi la uokoaji litachukua siku kadhaa kumalizika.
 

Duru za kitabibu zinasema kuwa waliofikishwa katika hospitali wengi wao Wafanyakazi kutoka kiwanda cha nguo na kuwa idadi ya waliopoteza maisha huenda ikaongezeka kwa kuwa hali ya baadhi ya Majeruhi ni mbaya na kuwa Hospitali imeomba kufanyika zoezi la kuchangia damu haraka.
 

Baadhi ya Wafanyakazi wamesema kuwa Jengo hilo lilionekana kuwa na nyufa siku ya jumanne na kufanya Wafanyakazi kuanza kuondoka kwenye Jengo hilo hata hivyo walilazimishwa na Waajiri wao kurudi tena kuendelea na kazi.
 

Manusura wa ajali hiyo wanasema saa moja baada ya kurejea kazini na kuanza kazi Jengo lilianza kutikisika hatimae kuanguka.
 

Waziri wa mambo ya ndani wa Bangladesh Muhiuddin Khan amesema kuwa Jengo hilo lilikuwa limejengwa kinyume cha Sheria na kwa kukiuka Sheria ya Ujenzi.
 

Bangladesh ni nchi ya pili kwa kuwa na viwanda vikubwa vya nguo duniani, ikiwa na masoko yake katika nchi za magharibi,lakini imekuwa ikikumbwa na ajli za namna hiyo sambamba na changamoto za Maandamano ya Wafanyakazi wanaodai nyongeza ya Mshahara na Mazingira mazuri ya kazi.
 

Mwezi Novemba mwaka jana, moto mkubwa ulijitokeza katika kiwanda cha nguo nje ya mji wa Dhaka ambapo Wafanyakazi 111 wa Kiwanda hicho walipoteza maisha.