Marekani

Jiji la NewYork nchini Marekani lakabiliwa na tishio la kushambuliwa kwa Bomu

Mtoto akiomboleza baada ya Shambulio la Bomu jijni Boston nchini marekani
Mtoto akiomboleza baada ya Shambulio la Bomu jijni Boston nchini marekani REUTERS/Jim Bourg

Jeshi la Polisi nchini Marekani katika Jiji la New York limetoa taarifa ya kueleza walikuwa wanawasaka kwa udi na uvumba ndugu wawili waliotekeleza shambulizi kwenye Mji wa Boston kutokana na wao kuwa na mpango wa kushambulia eneo la Times Square. 

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Polisi katika Jiji la New York Raymond Kelly amewaambia wanahabari walikuwa wanamsaka Dzhokhar Tsarnaev kutokana na kuwa na taarifa zake tangu mwaka jana wakiwa na mpango wa kutaka kushambulia eneo la Times Square.

 

Meya wa Jiji la New York Michael Bloomberg amesisitiza kuwa wataendelea kutumia kamera ambazo zimekuwa zikiwekwa kwenye mitaa ya Jiji hilo kwani ndizo zimesaidia kutambuliwa kwa wale walitekeleza mashambulizi kule Boston.

Watuhumiwa wa mashambulizi ya Boston Dzhokhar Tsarnaev na Tamerlan Tsarnaev wanatajwa tangu mwaka elfu mbili na kumi na mbili wamekuwa na mkakati kuandaa mashambulizi ya kujitoa mhanga katika Jiji la New York.

Bloomberg amewaambia waandishi wa habari kuwa wamepokea Taarifa kutoka shirika la upelelezi, FBI kuwa wamepata taarifa kutoka kwa mmoja kati ya waliotekeleza shambulio kuwa mji utakaoshambuliwa ni New York.

Watu watatu waliuawa kwa bomu jijini Boston wakati wa mashindano ya mbio za Marathon huku wengine 264 wakijeruhiwa.