Sudani

Sudani yanyooshewa kidole kuwa imempa Makazi Kiongozi wa Waasi wa LRA, Joseph Kony

Kiongozi wa Jeshi la uasi, LRA, Joseph Kony
Kiongozi wa Jeshi la uasi, LRA, Joseph Kony

Sudan imenyooshewa kidole kuwa imekuwa ikimpatia hifadhi Kiongozi wa Jeshi la waasi wa Lord's Resistance Army LRA Joseph Kony, Ripoti ya Shirika moja nchini Marekani imeeleza.

Matangazo ya kibiashara

Kony, Kiongozi wa LRA anayeshutumiwa kuwaajiri Watoto kwenye Jeshi lake akiwatumia kama Wapiganaji na kuwanyanyasa kijinsia ameendesha uasi nchini Uganda dhidi ya Serikali ya nchi hiyo kwa kipindi cha takriban Miaka 25.
 

Kony na Viongozi wenzake wanakabiliwa na mashtaka juu ya makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadam katika Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC.
 

Kwa mujibu wa Ripoti iliyotolewa hii leo, jeshi nchini Sudani limempatia hifadhi Kony tangu mwaka 2009 mpaka mwanzoni mwa mwaka huu.

Ripoti hiyo pia imeambatanisha picha za Satelaiti za kambi ya LRA, ambapo Kony alionekana mara ya misho mwaka 2012 katika mamlaka ya Sudan katika eneo linalopakana na Sudani kusini.
 

Shirika hilo la utafiti limetoa wito kwa jumuia ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, kuishinikiza Sudan kutoa ushirikiano katika juhudi za kupambana na LRA.
 

Mwanzoni mwa mwezi huu Marekani ilitangaza kutoa kitita cha dola milioni 5 kwa yeyote atakayewezesha kukamtwa kwa Kony.