DRC-UN

Kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa tayari kupambana, waasi waanza mazoezi ya kivita DRC

RFI

Kiongozi mkuu wa kikosi huru cha Umoja wa mataifa kitachotumwa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia, DRC kukabiliana na makundi ya waasi yanayotishia usalama katika eneo hilo Jenerali James Aloys Mwakibolwa amesema kuwa majeshi yake yako tayari kuanza kutekeleza majukumu yake katika eneo husika.

Matangazo ya kibiashara

Brigedia James Mwakibolwa ambae ni kutoka nchini Tanzania amesema hayo jana mjini Goma Wakati wa mazungumzo yake na Gavana wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini Julien Paluku Kahongya.

Jenarali Mwakibolwa amesema jana kuwa majeshi ya Umoja wa mataifa yameimarishwa na kwamba ana matumaini ya kufikia amani ya kudumu katika eneo la mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Hayo yanajiri Huku Vikosi vya wapiganaji waasi wa kundi la M23 vikisema kuwa wapo tayari kukabiliana na Majeshi hayo ya Umoja wa mataifa, na msemaji wao Vianey Kazarama akajitokeza na kusema kuwa Wanafanya mazoezi makali juu ya mbinu mpya za kupambana.

Waasi wa M23 wamekuwa wakipinga kupelekwa kwa kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kwa madai kuwa hatua hiyo inachochea vita zaidi katika eneo la Mashariki mwa DRC na badala yake waasi hao wanapendekeza suluhu ipataikane kupitia mazungumzo ya amani.

Kwa upande wake mashirika ya kiraia yanaunga mkono hatua ya kupelekwa kwa kikosi hicho na hivyo kuepusha ukiukwaji wa haki za binadamu wanaofanyiwa raia hususan wanawake ambao wameathiriwa na vitendo vya ubakaji.