MALI-UN

Mwanajeshi wa sita wa Ufaransa auawa katika mapambano nchini Mali

REUTERS/Carlos Barria

Mwanajeshi wa Sita kutoka Ufaransa ameuawa jana katika milima ya Ifoghas, wakati gari lililokuwa linawasafirisha kuelekea kwenye maeneo ya kaskazini mwa Mali lilipokanyaga bomu za kutegwa ardhini.

Matangazo ya kibiashara

Mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 32 aliyefahamika kuwa ni Koplo Stéphane Duval alikuwa miongoni mwa wanajeshi wa Ufaransa waliotumwa katika maeneo ya mpaka baina ya Mali na Algeria.

Thierry Burkhard ni msemaji wa Majeshi ya Ufaransa katika operesheni za huko Mali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo linatoa changamoto kwa wanajeshi wa Ufaransa katika kukabiliana na waasi hao.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametuma salama zake za rambirambi kwa familia ya mwanajeshi huyo na amengeza ushujaa wa wanajeshi wa Ufaransa katika operesheni hiyo ya kijeshi nchini Mali.

Tukio hilo linatokea huku serikali ya Ufaransa ikijipanga kuendeleza zoezi la kuwaondoa askari wake nchini Mali na kupisha majeshi ya kimataifa kuendeleza operesheni hiyo kwenye eneo la Kaskazini mwa nchi ya Mali.

Ufaransa imeanza kuwaondoa wanajeshi wake 4,500 ambapo kati yao watabaki wanajeshi 1,000 kuungana na jeshi la kimataifa na watakua huko mpaka zaidi ya mwisho wa mwaka huu.
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wapatao 12,600 walioidhinishwa wiki iliyopita na umoja huo kwenda nchini Mali watakua na jukumu la kulinda amani na kuirejesha Kaskazini Mali katika hali yake ya kawaida.
Wanajeshi hao wataanza kupelekwa Mali kwa awamu kuanzia mwezi Julai mwaka huu huku jeshi la Ufaransa likiwa tayari limesambaratisha ngome waasi wa vikundi vya kiislam ingawaje bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi madogo madogo.