SYRIA-UMOJA WA NCHI ZA KIARABU-UN

Mjumbe wa UN Lakhdar Brahimi kubwaga manyanga usuluhishi wa mgogoro wa Syria?

Mpatanishi wa mgogoro wa Syria nchini ya Umoja wa Mataifa UN, Lakhdar Brahimi anatarajia kujiuzulu kufuatia kuwepo kwa mvutano miongoni mwa Jumuia ya kimataifa katika jitihada za kumaliza machafuko ya Syria.

UN Photo/Evan Schneider
Matangazo ya kibiashara

Brahimi aliyechukua nafasi ya Kiongozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan mwezi Agosti mwaka jana anataka kujiuzulu, hata hivyo ameshawishiwa kusubiri kwa siku kadhaa.
 

Kama ilivyokuwa kwa Annan, Brahimi amekuwa akionesha kutofurahishwa na mgawanyiko ndani ya Umoja wa Mataifa juu ya Syria, Urusi ikiunga mkono Utawala wa Rais wa Syria, Bashar Al Assad, huku mataifa ya Magharibi na jumuia ya nchi za ghuba zikiunga mkono upinzani.
 

Wakati huo huo Marekani imeapa kupata ukweli juu ya shutma kuwa utawala wa Rais Assad nchini Syria unatumia Silaha za kemikali kupambana na Waasi nchini humo kabla ya kuchukua hatua zaidi.
 

Hata hivyo hatua imepingwa vikali na serikali ya Syria kupitia kwa Balozi wa Syria ndani ya Umoja wa Mataifa, Bashaar Jafaari.
 

Serikali ya Marekani tayari imeviagiza vyombo vyake vya usalama kuandaa hatua za kuchukua baada ya nchi hiyo kujiridhisha na ushadi kuhusu majeshi ya Syria kutumia silaha za kemikali.