SYRIA-UMOJA WA MATAIFA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon akerwa na mashambulizi ya Israeli kulenga vituo vya kijeshi vya Syria

Mashambulizi ya angani ya ndege za Israeli nchini Syria yamesababisha kuharibiwa kwa vituo vya kijeshi vya Utafiti huko Damascus
Mashambulizi ya angani ya ndege za Israeli nchini Syria yamesababisha kuharibiwa kwa vituo vya kijeshi vya Utafiti huko Damascus REUTERS

Mashambulizi ya angani ambayo yametekelezwa na ndege za Israeli nchini Syria yamempa wasiwasi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ambaye anahisi hatua hiyo itazorotesha juhudi za kurejesha amani katika Taifa hilo lililo kwenye vita kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa UN Ban amesema mashambulizi hayo yaliyolenga Vituo vitatu vya Utafiti wa Kijeshi Jijini Damascus yataongeza hali ya hofu na hata kuchochea machafuko zaidi kutokana na vita hivyo kuanza kuingiliwa na majirani ambao wanaweza wakachangia umwagaji zaidi wa damu.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN Martin Nesirky amesema Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka pande zote kuonesha utulivu ili kusaidia juhudi za kupatikana kwa amani iliyopotea kwa zaidi ya miaka miwili na kuchangia zaidi ya watu laki moja kupoteza maisha.

Nesirky akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ban amesema haya yanayofanywa sasa yanaweza yakachangia Syria kuendelea kuwa kaburi kitu ambacho kimekuwa kikipingwa vikali na Umoja wa Mataifa UN unaofanya juhudi za kusaka suluhu.

Serikali ya Syria inayoongozwa na Rais Bashar Al Assad imelaani vikali shambulizi hilo na kueleza kilichofanyika ni kama tangazo la vita kati yake na jirani zao wa Israeli na hivyo hawataacha suala hilo lipite hivi hivi bila ya wao kujibu mashambulizi.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nazo zimelaani shambulizi hilo lililotekelezwa na ndege za Israeli katika ardhi ya Damascus na imetaka mikataba ya kimataifa iheshimiwe kuhusiana na suala la mipaka ya nchi na hivyo shambulizi hilo halikubaliki.

Serikali ya Israeli imekuwa mstari wa mbele kuwatuhumu Wapiganaji wa Kundi la Hezbollah kutoka nchini Lebanon wakidai wanashirikiana na wanajeshi wa serikali ya Syria ambao wamekuwa wakipata msaada wa kisilaha kutoka Iran na kuendelea na mashambulizi.

Shambulizi hili la angali lililolenga ghala moja la silaha huko Damascus lunakuja wakati huu ambapo Msuluhishi wa mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi akitanhaza kujiuzulu wadhifa wake mwishoni mwa mwezi huu wa May.