MALAYSIA

Upinzani wapinga matokeo ya Uchaguzi nchini Malaysia huku Waziri Mkuu Najib akiahidi kusimamia maridhiano baada ya ushindi

Viongozi wa Muungano wa Barisal ambao wameshinda kwenye Uchaguzi Mkuu nchini Malaysia
Viongozi wa Muungano wa Barisal ambao wameshinda kwenye Uchaguzi Mkuu nchini Malaysia

Muungano wa Vyama Tawala nchini Malaysia umefanikiwa kushinda kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika jana na kufanikiwa kuendelea kusalia madarakani baada ya kuongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka hamsini na sita.

Matangazo ya kibiashara

Muungano huo unatambulika kwa jina la Barisan Nasional umefanikiwa kushinda uchaguzi huo na kutoa ahadi ya kuhakikisha wanaleta maridhiano baina ya wananchi wa Taifa hilo ambalo limeanza kugawanyika katika misingi ya kisiasa.

Matokeo hayo ya ushindi ulioelekea Muungano wa Barisan Nasional umepingwa vikali na Muungano wa Upinzani unaoongozwa na Anwar Ibrahim ambao wanadai kumekuwa na njama na hila kwenye uchaguzi huo na hivyo hawatambui matokeo hayo.

Ibrahim amesema Muungano wa Barisal ambao unaongoza serikali umefanya ulaghai kwenye uchaguzi huo na hivyo kushindwa isivyo halali na watandelea kupinga matokeo hayo wakitaka haki itendeke kwenye hili.

Kiongozi huyo wa Muungano wa Upinzani ameilaumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushindwa kufanyakazi yake ipasavyo na badala yake imekubali kuhusika kwenye kuvurugwa kwa uchaguzi huo muhimu.

Licha ya Muungano wa Upinzani kukataa matokeo hayo lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeutangaza Muungano wa Barisan kuwa mshindi kutokana na kupata wingi wa viti Bungeni dhidi ya Upinzani.

Waziri Mkuu Najib Razak ndiye anaongoza Muungano wa Barisal kufuatia ushindi ambao wameupata kwenye uchaguzi huo anatarajiwa leo kupata ridhaa ya kuunda serikali mpya ambayo itaongoza nchi ya Malaysia.

Muungano wa Barisal umepata viti 133 huku Upinzani ukiambulia vita 89 pekee kati ya nafasi 222 za wabunge katika Bunge la nchi hiyo na tayari Waziri Mkuu Najib amesema maridhiano ndiyo silaha yake mpya.

Muungano wa Upinzani unaongozwa na Anwar licha ya kulalama kufanyiwa hila kwenye uchaguzi huo lakini wamefanikiwa kuongeza viti 14 kwenye Bunge na kufikisha idadi ya viti 89 tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Wachambuzi wa Siasa nchini Malaysia wametabiri Waziri Mkuu Najib anatakiwa awe makini katika uongozi wake ili awaunganishe wananchi na kama atashindwa kufanya hivyo basi itakuwa vigumu kwake kuweza kuongoza inavyostahili.