SYRIA-UMOJA WA MATAIFA

Waasi nchini Syria watuhumiwa kutumia silaha zenye sumu ya sarin kwenye vita dhidi ya Majeshi ya Serikali ya Rais Assad

Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa UN imebaini wapiganaji wa Upinzani nchini Syria ndiyo wanatumia silaha za kemikali kwenye vita vyao dhidi ya Serikali ya Rais Bashar Al Assad kulingana na uchunguzi uliofanywa kwa waathirika na Madaktari. Mjumbe wa Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa Carla Del Ponte ndiye ametoa kauli hiyo kwa kusema wamebaini waasi wanatumia sumu aina ya sarin inayotumika kwenye kama moja ya kemikali ambazo zitaunda silaha za maangamizi.

Mjumbe wa Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa Carla Del Ponte akitangaza hatua ya kutambua Waasi wanatumia gesi yenye sumu ya sarin nchini Syria
Mjumbe wa Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa Carla Del Ponte akitangaza hatua ya kutambua Waasi wanatumia gesi yenye sumu ya sarin nchini Syria
Matangazo ya kibiashara

Del Ponte ameeleza ushahidi wa kutosha umekusanywa kuthibitisha matumizi hayo ya kemikali kwenye vita vya Syria ambapo waasi wanatumia sumu aina ya sarin katika kupambana na Wanajeshi wa Serikali ya Damascus.

Mjumbe huyo wa Kamati ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa amesema japokuwa hawajapata uthibitisha wa mwisho lakini uchunguzi uliofanywa na Madaktari umebaini waasi ndiyo wanatumia sumu hizo kwenye mapambano yao.

Del Ponte amebainisha kwa sasa wamekuwa na ushahidi unaoonesha gesi hiyo ya sumu ya sarin inatumiwa na upinzani pamoja na waasi na si serikali kama ambavyo ilikuwa inatuhumiwa hapo kabla.

Mwanamama huyo amesema hizi si taarifa za kushangaza kutokana na upinzani kuanza kupata ufadhili wa mataifa ya kigeni hivyo inawezekana kabisa wakawa wanapewa gesi hiyo waitumie kwenye vita hivi.

Mjumbe wa Kamati ya Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa Del Ponte amesema pia hawajapuuza madai ya kwamba serikali nayo inatumia silaha za kemikali lakini ukweli kwa sasa umebaini waasi ndiyo wanatumia silaha hizo.

Ushahidi huu mpya unaweza ukaiacha njia panda serikali ya Marekani iliyokuwa tayari kuchukua hatua iwapo kungekuwa na ushahidi ya kwamba serikali ya Rais Assad ndiyo inatumia silaha hizo za kemikali.

Uchunguzi huu umefanyika licha ya kwamba serikali ya Damascus kuendelea kuwazuia wajumbe wa Tume ya Uchunguzi kuingia katika ardhi ya taifa hilo kufanya uchunguzi kubaini kama kweli kumekuwa na matumizi ya silaha za kemikali.

Serikali ya Damascus ilikuwa inatuhumiwa kutumia silaha za kemikali licha ya Viongozi wake wa juu kujitokeza mara kadhaa na kukanisha vikali madai hayo wakisema hawezi kutumia silaha hizo kwenye vita vya ndani licha ya kumiliki silaha hizo.