Watu 6 wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika kwenye shambulizi lililotekelezwa katika Kanisa la Mtakatifu Joseph
Jeshi la Polisi nchini Tanzania liwashikilia watu sita wakihusishwa na shambulizi lililotekelezwa kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph maeneo ya Olasit Mkoani Arusha na kusababisha vifo vya watu wawili na kuwaacha wengine zaidi ya thelathini wakijeruhiwa. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daktari Emmanuel Nchimbi akiwa Dodoma ndiye ametangaza kukamatwa kwa watuhumiwa hao sita wa kwanza kipindi hiki msako kklai ukiendelea kuwaska waliopanga na hatimaye kutekeleza shambulizi hilo linalodaiwa kuwa ni bomu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Waziri Daktari Nchimbi amesema ameshatoa maagizo kwa Mamlaka husika kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina kubaini wale waliofanya shambulizi hilo ambalo limetia dosari hali ya utulivu wa Tanzania ambayo imekuwa ikijivunia kwa miaka mingi na kupata heshima kubwa.
Makamu wa Rais Daktari Mohamed Gharib Bilali aliwasili mkoani Arusha na kwenda kuwafariji majeruhi wa shambulizi hilo baya na kueleza serikali imejiapiza kuhakikisha inawasaka na hatimaye kuwatia nguvuni wale wote ambao wamehusika kwa namna moja ama nyingine kwenye shambulizi hilo.
Daktari Bilali amewataka wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kipindi hiki ambacho uchunguzi unaendelea kufanyika kuwabaini waliopanga na hata wale waliotekeleza shambulizi hilo lililokwamisha kufanyika kwa uzinduzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph.
Sherehe hizo zilingia dosari na kusababisha kuahirishwa kwa uzinduzi huo wa Kanisa la Mtakatifu Joseph ambao ulihudhuriwa na Balozi wa Vatican nchini Tanzania Askofu Francisco Montecillo Padilla ambaye hakupata madhara ya aina yoyote.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo aliwaambia wanahabari kwa sasa hawatakiwi kuanza kubashiri kina nani ambao wamehusika kwenye shambulizi hilo na badala yake waliachie Jeshi la Polisi kufanyakazi yake kisha taarifa rasmi itatolewa kujua chanzo chake.
Mulongo amekataa tukio hilo kuhusishwa na mashambulizi ambayo yamekuwa yakitokea nchini Tanzania kwa kuchomwa kwa makanisa na hata kushambuliwa kwa Viongozi wa kidini na badala amesema hili ni tukio tofauti kabisa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas amethibitisha kupokelewa kwa majeruhi zaidi ya thelathini kati hao watatu wakiwa katika hali mbaya zaidi na wanaendelea kupatiwa huduma.
Naye Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema amelaani vikali shambulizi hilo na amekataa kuhusishwa na mgogoro wa kidini wala kisiasa na badala yake uchunguzi ufanyike ili kupata chanzo cha shambulizi hilo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye yupo ziarani nchini Kuwait ametuma salamu za pole kwa wale wote walioathirika na shambulizi hilo baya na kuagiza mamlaka husika kuhakikisha waliohusika wanakutana na mkono wa sheria.