DRC-UMOJA WA MATAIFA

Mjumbe Maalum wa Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR Mary Robinson aomba Kikosi kitakachopelekwa DRC kupambana vilivyo na Makundi yanayomiliki Silaha

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa UN Mary Robinson akiwa Mashariki mwa DRC kukutana na waathirika wa vita inayoendelea
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa UN Mary Robinson akiwa Mashariki mwa DRC kukutana na waathirika wa vita inayoendelea UN Photo/Sylvain Liechti

Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR Mary Robinson ametoa wito kwa Kikosi Maalum cha Umoja huo kitakachopelekwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kuhakikisha kinakabiliana haswa na Makundi yanayomiliki silaha.

Matangazo ya kibiashara

Robinson ametoa ushauri hiyo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC na kuongeza iwapo Kikosi hicho maalum hakitafanyakazi yake ipasavyo ni wazi kabisa amani katika eneo la Mashariki mwa DRC itaendelea kuwa kitendawili kilichokosa jibu.

Mjumbe huyo Mpya kwenye Eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR amekiri anahofi kama hakutakuwa na mkakati madhubuti kwenye operesheni hiyo maelfu ya wananchi wanaweza wakakwama kwenye sehemu hizo za mapigano na kujikuta wakiathirika zaidi.

Robinson ameliambia Baraza la Usalama kwenye operesheni hii lazima iangalie suala la huduma muhimu za binadamu kwa wakazi wa Mashariki mwa DRC ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiteseka kutokana na uwepo wa mapigano yasiyokwisha.

Kauli ya Robinson mbele ya Baraza la Usalama imekuja baada ya yeye kufanikiwa kuzuru katika eneo la Mashariki na kujionea madhira wanayokumbana nayo wananchi ikiwepo ubakaji, kukimbia makazi yao sambamba na ukosefu wa usalama wa kudumu.

Mjumbe huyo ameliambia Baraza la Usalama Jumuiya zinazoshughulikia masuala ya kibinadamu katika nchi za Rwanda, Uganda na Burundi zimeonekana kuguswa na kile ambacho kinaendelea Mashariki mwa DRC na wametaka Umoja wa Mataifa UN kuwa makini wakianza operesheni yao.

Robinson pia hakuliacha Kundi la Waasi la M23 ambalo limekuwa chanzo cha kuzorota kwa usalama na kutaka nalo lishughulikiwe kwani hiyo inaweza ikasaidi pakubwa kurejesha utulivu katika nchi ya DRC.

Kundi la Waasi la M23 ambalo siku ya jumatatu limeadhimisha mwaka mmoja tangua kuazisha mapigano na Jeshi la Serikali FARDC limekuwa likinyooshewa kidole cha lawama kwa kuchangia uwepo wa machafuko Mashariki mwa DRC.

Robinson ameliomba Baraza la Usalama kuweka maani kwenye operesheni yao kuhakikisha linakabiliana na Kundi la Waasi la M23 ambalo ni miongoni mwa makundi yanayomiliki silaha kinyume cha sheria nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.