SOMALIA-UINGEREZA

Mkutano wa kujadili mustakabli mwema wa nchi ya Somalia waanza nchini Uingereza na kuzileta pamoja Nchi 50

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akitafakari jambo kabla ya kuanza kwa mkutano wa kuisaidia kuijenga nchini yake Jijini London, Uingereza
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akitafakari jambo kabla ya kuanza kwa mkutano wa kuisaidia kuijenga nchini yake Jijini London, Uingereza

Mkutano wa kujadili na kusaidia ustawi na kudumishwa kwa amani nchini Somalia unaanza hii leo ambapo nchi hamsini zinashiriki pamoja na Taasisi zisizo za Kiserikali katika Mkutano unaofanyika Jijini London nchini Uingereza.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo unafanyika huku ukibeba agenda inayotaka kuliona taifa hilo likistawi baada ya kupita katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vinaratibiwa na Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab.

Mataifa haya yanakutana yakiwa na matumaini wanaweza wakaibuka na mikakati madhubuti ya kuhakikisha maendeleo yanapatikana baada ya kusambaratishwa kwa Kundi la Wanamgambo wa Al Shaba kwenye ngome zao.

Mkutano huo utakuwa unaongozwa na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud wakitaka kuhakikisha nchi hiyo inajijenga upya na kuimarika kiuchumi.

Miongoni mwa Mashirika ambayo yamealikwa kwenye mkutano huo ni pamoja na Umoja wa Mataifa UN, Umoja wa Afrika AU, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF pamoja na Mashirika mengine kutoka nchi jirani na Somalia.

Rais wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria Mkutano huo ambapo nchi yake ni miongoni mwa sehemu mwa Jeshi la Umoja wa Afrika AMOSIM lililofanikisha kuangushwa kwa ngome za Al Shabab.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imetoa muhtasari wa kile ambacho kitajadiliwa na kueleza watafanya kila linalowezekana kuisadia nchi ya Somalia kuweza kupiga hatua baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe wa wenyewe vilivyodumu kwa miaka ishirini na moja.