BANGLADESH-UMOJA WA MATAIFA

Upinzani nchini Bangladesh waitisha maandamano ya siku mbili kupinga mauaji yaliyofanywa dhidi ya Waumini wa Kiislam

Polisi nchini Bangladesh wakipambana na Waumini wa Kiislam walioandamana kutaka uwepo wa sheria madhubuti ya kukabiliana na wale wanaokufuru
Polisi nchini Bangladesh wakipambana na Waumini wa Kiislam walioandamana kutaka uwepo wa sheria madhubuti ya kukabiliana na wale wanaokufuru REUTERS/Andrew Biraj

Vyama vya Upinzani nchini Bangladeshi vimeitisha maandamano ya kitaifa ya siku mbili yatakayoanza siku ya jumatano kuonesha kuguswa kwao na vifo vilivyosababishwa na mapambano baina ya Waumini wa Kiislam na Jeshi la Polisi.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani nchini Bangladeshi umesema wanataka kuonesha hasira zao kutokana na mauaji ya watu arobaini na tisa yaliyofanywa na Vyombo vya Usalama pale walipotumia nguvu kubwa kuzima maandamano ya Waumini wa Kiislam yaliyoanza mchana wa jumapili.

Chama Kikuu Cha Upinzani cha BNP kwa kushirikiana na Vyama vingine vya Kiislam ndiyo vimeitisha maandamano hayo ambayo athari zake zimewaacha zaidi ya mamia ya Waumini wa Kiislam wakijeruhiwa vibaya.

Msemaji wa Chama Cha BNP Khandaker Mosharraf amesema maandamano hayo ya siku mbili yanakuja kuonesha kukerwa kwake na kutekelezwa kwa mauaji hayo ya umma ambayo yametia dosari utulivu wa Taifa hilo.

Maandamano haya yanaitishwa huku serikali ikitangaza kuwafungulia mashtaka wanaharakati wapatao 194 kutoka Kundi la Hefajat-e-Islam ambao wanatajwa kuandaa maandamano hayo yaliyodumu kwa siku mbili mfululizo.

Msaidizi wa Inspekta wa Jeshi la Polisi Tabibur Rahamn amesema Katibu Mkuu wa Kundi la Hefajat-e-Islam Junayed Babu Nagori ni miongoni mwa wale waliofunguliwa mashtaka ikiwemo ya mauaji.

Kiongozi wa Kundi la Hefajat-e-Islam mwenye umri wa miaka 90 Allama Ahmad Shafi ameendelea kulindwa vilivyo na wafuasi wake ili asiweze kutiwa nguvuni na Jeshi la Polisi nchini Bangladesh linalimsaka kwa udi na uvumba.

Polisi imesema watu wapatao laki mbili ambao ni waumini wa Kiislam waliandamana wakishinikiza serikali ya Bangladesh kuibuka na sheria ya kukufuru ambayo itakuja na hukumu ya kunyongwa kwa wale watakaokutwa na hatia bila kujali imani yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ametaka kumalizwa kwa machafuko hayo na kueleza namna ambavyo amesikitishwa na hatua ya wananchi wengi kupoteza maisha kwenye vurugu hizo.

Msemaji wa Katibu Mkuu Ban, Martin Nesirky amesema Kiongozi huyo anataka uwepo utayari wa kushughulikia tatizo hilo kwa kuwahusisha Viongozi wa Kisiasa na wale wa kidini.