NIGERIA

Kundi la Boko Haram lashambulia Kambi ya Jeshi nchini Nigeria kwenye tukio lililosababisha vifo vya watu 55

Kambi ya Jeshi nchini Nigeria katika Mji wa Bama ambayo imeshambuliwa na Kundi la Boko Haram
Kambi ya Jeshi nchini Nigeria katika Mji wa Bama ambayo imeshambuliwa na Kundi la Boko Haram

Wanamgambo wa Kundi la Boko Haram nchini Nigeria wakiwa wamejihami kwa silaha madhubuti za kivita wamevamia Kambi ya Jeshi na kisha kuzuka mapigano makali yaliyosababisha vifo vya watu 55 huku wafungwa 105 wakitoroka.

Matangazo ya kibiashara

Uvamizi huo wa Kundi la Boko Haram umefanyika katika Mji wa Bama uliopo Jimboni Maiduguri ambapo wanamgambo hao walifanya shambulizi kwenye Kambi hiyo ya Kijeshi na tayari Jeshi nchini hilo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo baya.

Msemaji wa Jeshi katika Jimbo la Maiduguri Musa Sagir amesema hilo ni shambulizi la kigaidi lililotekelezwa na Wanamgambo wa Kundi la Boko Haram ambao wamekuwa wakipingana na Utawala uliopo madarakani.

Jeshi la Polisi limesema katika kujibu mashambulizi hayo ya uvamizi wa Wanamgambo wa Boko Haram walifanikiwa kuwaua wanamgambo kumi huku mmoja akikamatwa wakati akijiandaa kukimbia.

Miongoni mwa wale 55 waliopoteza maisha ni pamoja na wanajeshi wawili, wafungwa waliokuwa wanashikiliwa kwenye kambi hiyo, askari polisi na raia wengine wa akawaida waliokuwa eneo hilo la Kambi ya Jeshi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi huko Maiduguri Sagir amesema walinzi wa gereza 14 wameuwawa, wanajeshi wawili, askari polisi waliopoteza maisha ni 22, raia wa kawaida 4 pamoja na wanamgambo wa Boko Haram 13.

Shambulizi hilo la kigaidi kama ambavyo limetafsiriwa na Jeshi limeacha madhara makubwa ikiwemo kuchomwa kwa magari ya jeshi sambamba na kushambuliwa na kuharibiwa vibaya kwa Zahanati ya jeshi hilo.

Boko Haram wamefanya shambulizi hili huku kukiwa na kumbukumbu za kuwepo kwa mfulilizo wa mashambulizo yaliyochangia vifo vya watu 17 huku nyumba kadhaa zikitekezwa kwa moto.

Kundi la Boko Haram tangu mwaka 2009 limekuwa mstari wa mbele kutekeleza mashambulizi ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu tatu wakipinga uwepo wa elimu ya magharibi nchini Nigeria.