URUSI-SYRIA-MAREKANI

Lakhdar Brahimi apongeza uamuzi wa Marekani na Urusi kufikia makubaliano ya kumaliza umwagaji wa damu nchini Syria

Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria anayetambuliwa na Umoja wa Mataifa UN na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Lakhdar Brahimi amepokea kwa mikono mawili makubaliano yaliyofikiwa baina ya Marekani na Urusi ya kuhakikisha yatashirikiana kumaliza mzozo unaoendelea huko Damascus. Brahimi kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake amesema hatua ya mataifa hayo mawaili kufikia muafaka kusaka mbinu za kumaliza umwagaji wa damu uliodumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili ni cha kipekee na kinaweza kikasaidia kurejea kwa utulivu nchini Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry akiwa kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry akiwa kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov
Matangazo ya kibiashara

Mpatanishi huyo wa Mgogoro wa Syria ameeleza taarifa hizo za makubaliano zimekuwa ni njema na zinaleta matumaini ya kupatikana suluhu muafaka ya umwagaji wa damu unaoendelea kugharimu maisha ya wananchi wasio na hatia katika Taifa hilo.

Brahimi ameweka bayana makubaliano hayo yatasaidia pakubwa kurejea kwa utulivu katika ukanda mzima kitu ambacho kitakuwa kichocheo tosha kabisa cha kupatika hali ya usalama nchini Syria iliyotoweka tangu waasi walipoanzisha mapambano yakilenga kuiangusha serikali ya Rais Bashar Al Assad.

Kauli ya Brahimi imekuja baada ya mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka Marekani na Urusi kukutana na hatimaye majadiliano yao kuzaa matunda kwa kuafikiana kushirikiana katika kuhakikisha umwagaji wa damu nchini Syria unakoma haraka iwezekanavyo.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika usiku wa jumanne na kudumu kwa muda wa zaidi ya saa mbili na nusu hatimaye yaliyaleta pamoja mataifa hayo mawili yaliyokuwa na sera tofauti juu ya mgogoro unaoendelea nchini Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alijitokeza mbele ya wanahabari na kusema wamekubaliano na Marekani kuhakikisha mgogoro wa Syria unamalizwa kwa njia za kisiasa na hivyo wataikutanisha serikali na wapinzani kwenye meza ya mazungumzo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema taifa lake pekee haliwezi kumaliza machafuko yanayoendelea knchini Syria lakini kwa kupata ushirikiano kutoka Urusi hilo linaweza likafanikiwa.

Mkutano huu umekuja huku Marekani hapo awali ikiwa na mpango wa kuwasaidia Wapinzani kwa kuwapa silaha wakishirikiana na Uingereza na Ufaransa hatua iliyokuwa inapingwa vikali na Urusi kwa kushirikiana na China.

Urusi na China ndiyo watetezi pekee wa Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC ambao walikuwa wanapingana na mikakati iliyokuwa inaongozwa na Marekani pamoja na washirika wao ambao walikuwa wanataka njia za kijeshi ndiyo zitumike kusaka suluhu.