PAKISTAN

Mwanasiasa Imran Khan afya yake imeimarika baada ya kupatiwa matibabu kufuatia kuanguka jukwaani

Mwanasiasa mahiri nchini Pakistani Imran Khan aliyeanguka jukwaani akiendelea na kampeni zake za kunadi sera anaendelea kupatiwa matibabu hospital kufuatia kupata majeraha kichwani na sasa hali yake inaendelea vyema.

Mwanasiasa Imran Khan akiwa hospitali akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kuanguka jukwaani akiwa kwenye kampeni Jijini Lahore
Mwanasiasa Imran Khan akiwa hospitali akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kuanguka jukwaani akiwa kwenye kampeni Jijini Lahore
Matangazo ya kibiashara

Picha za Televisheni zimemuonesha Khan akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kuanguka akiwa jukwaani lakini mwenyewe ameendelea kupiga kampeni zake akiwa anaendelea kutibiwa.

Khan ambaye ni mchezaji wa zamani wa mchezo wa kriketi amewataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la upigaji kura litakalofanyika nchini Pakistan siku ya jumamosi hii.

Mwanasiasa huyo kutoka Chama Cha PTI amelazwa katika Hospital ya Shaukat Khanum ambapo Msemaji wa Hospital hiyo amesema hali ya Khan imeimarika japokuwa bado madaktari wanaendelea kutoa tiba.

Khan anayewania ubunge katika Jimbo la Lahore amesema amekuwa akifanya kila linalowezekana kwa ajili ya kuikoa nchi yake na ndiyo maana anafanya kampeni licha ya kwamba hali yake kiafya kuzorota.

Msemaji wa Chama Cha PTI Shirin Mazari amesema sehemu ambayo ameumia Khan ni kwenye paji lake la uso lakini inawezekana akarejea kwenye kampeni zake kabla ya kufungwa na kura zikapigwa.

Khan alianguka jukwaani akiwa kwenye kampeni zake na hili linakuja baada ya mwanasiasa huko kukaidi agizo la madaktari wake ambao walimtaka apumzike kutokana na afya yake kuzorota.

Pakistan inapitia kwenye kipindi cha mashambulizi ya kujitoa mhanga kwa sasa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi siku ya jumamozi huku takwimu zikonesha zaidi ya watu mia moja wamepoteza maisha kwenye mashambulizi hayo.