TANZANIA-DRC-UMOJA WA MATAIFA

Kikosi cha Tanzania chaelekea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kulinda amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa UN

Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi bendera Kiongozi wa Batalioni inayoelekea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kulinda amani
Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi bendera Kiongozi wa Batalioni inayoelekea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kulinda amani

Kikosi cha kwanza cha Wanajeshi wa Tanzania kinachoenda Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kulinda amani na kukabiliana na Makundi ya Waasi kinaondoka siku ya alhamisi kikiwa na jumla ya wanajeshi 1,280. Wanajeshi hao watanzania wataungana na wenzao kutoka Malawi na Afrika Kusini huko Mashariki mwa DRC wakiwa na jukumu la kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana baada ya eneo hilo kuwa hatari kwa wakazi wake.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jakaya Mrisho Kikwete amewakabidhi bendera wanajeshi hao na kuwataka waendeleze utamaduni wa jeshi hilo kwenye shughuli zake za ulinzi wa amni.

Rais Kikwete amewataka wanajeshi hao kuwa na nidhamu na utii ili kuhakikisha wanaendelea kulinda heshima yao wenyewe na heshima ya nchi ambayo imekuwa ikiaminika katika Jumuiya ya Kimataifa.

Kikosi hiki cha wanajeshi wa Tanzania kitakuwa sehemu ya wanajeshi 2,500 wa Umoja wa Mataifa UN ambao watapelekwa Mashariki mwa DRC kukabiliana na makundi yanayomiliki silaha yanayotajwa kuwa chanzo cha kuzorota kwa amni.

Miongoni mwa makundi ambayo yakabiliwa na nguvu hiyo ya Kikosi Maalum cha Umoja wa Mataifa kinachopelekwa kupambana na makundi yanayomiliki silaha ni pamoja na Kundi la Waasi la M23.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC lilipitisha azimio la kupelekwa kwa kikosi cha kupigana Mashariki mwa DRC kutokana na kulaumiwa pakubwa kushindwa kuchukua hatua huku damu ikiendelea kumwagika katika eneo hilo.

Umoja wa Mataifa UN ulianza kukosolewa kutokana na Kikosi chake cha kulinda aamani cha MONUSCO kushindwa kuwasaidia wananchi wanaoteseka kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Kundi la Waasi la M23.

Kiongozi wa Kisiasa wa Kundi la M23 Bertrand Bisimwa mwezi uliopita aladai kuliandikia barua ya onyo Bunge la Tanzania kutoidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi hao kwa sababu wao watakuwa tayari kuwashambulia watakapoanzisha mashambulizi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Camilius Membe akajitokeza na kukanusha vikali vitisho vyovyote ambavyo wamepokea kutoka kwa Kundi la Waasi la M23 na wao wanapeleka wanajeshi wao kama walivyopanga.

Kundi la Waasi la M23 ambalo lipo kwenye mazungumzo na Serikali ya Kinshasa yanayofanyika nchini Uganda limekuwa mstari wa mbele kutaka suluhu ipatikane kupitia mazungumzo na si mapigano.