PAKISTAN

Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Raza Gilani atekwa nyara kwenye kampeni za mwisho na watu wenye silaha

Watu wenye silaha nchini Pakistan wamemtekanyara mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa taifa hilo Yousuf Raza Gilani, Ali Haider Gilani katika siku ya mwisho ya kampeni kabla ya wananchi wa Taifa hilo hawajapiga kura siku ya jumamosi.

Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Yousuf Raza Gilani, Ali Haider Gilani ambaye ametekwa na watu wenye silaha
Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Yousuf Raza Gilani, Ali Haider Gilani ambaye ametekwa na watu wenye silaha
Matangazo ya kibiashara

Haider Gilani ametekwa katika Mji wa Multan baada ya kuzuka mashambulizi kwenye kampeni zake za mwisho na ndipo watu hao walimteka na kwenda naye kusikojulikana hadi sasa.

Familia ya Waziri Mkuu wa zamani Raza Gilani imekuwa na nguvu kubwa katika Chama cha Watu wa Pakistani PPP na wamekuwa wakisimama kidete kuhakikisha wanashinda viti vya kutosha Bungeni.

Kampeni za Chama cha PPP zilishapewa kitisho kutoka kwa Wanamgambo wa Taliban ya kwamba zitashambuliwa lakini hakuna hatua zozote madhubuti zilizochukuliwa kujikinga na tishio hilo.

Licha ya Wanamgambo wa Taliban kutoa kitishi hicho mapema lakini halijajitokeza na kuthibitisha iwapo linahusika na utekajinyara wa Haider Gilani kipindi hiki msako ukiendelea kufanywa.

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Raza Gilani kwa upande wake ametupa lawama kwa wapinzani wake kisiasa ambao anaamini wapo nyuma ya tukio hilo kwa kuliandaa na hatimaye kulitekeleza.

Raza Gilani ambaye mahasimu wake wa kisiasa wamekuwa wakitumia kila mbinu kuhakikisha wanamdhoofisha kisiasa lakini yeye ataendelea kukabiliana nao kwa njia zozote zile.

Afisa wa Polisi Khurram Shakur amewaeleza wanahabari watu wwaliojihami kwa silaha walifika na kushambulia mkutano huo siasa na kisha kumteka Haider Gilani na kutoroka naye kwenye gari jeusi.

Kaka yake Haider Gilani, Ali Musa amesema wanataka Jeshi la Polisi kufanyakazi yake ipasavyo na kuhakikisha ndugu yao anapatikana haraka iwezekanavyo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi siku ya jumamosi.

Duru za usalama zinasema mtu mmoja alipoteza maisha kwenye shambulizi hilo lililochangia utekwajinyara kwa Haider Gilani na tayari familia yake imetaka Jeshi la Polisi kuhakikisha kijana wao anapatikana akiwa hai.

Kundi la Wanamgambo wa Taliban limeshatishia kufanya mashambulizi siku ya uchaguzi huo ambao utafanyika siku ya jumamosi wakisema hawataki kufanyika kwa uchaguzi huo uliowatenga wao.