HAITI-UMOJA WA MATAIFA

Waathirika wa Ugonjwa wa Kipindupindu nchini Haiti kuufungulia kesi Umoja wa Mataifa UN kama utashindwa kuwalipa fidia

Waathiriwa wa ugonjwa wa kipindupindi nchini Haiti wakiwa kwenye makambi wakipata huduma
Waathiriwa wa ugonjwa wa kipindupindi nchini Haiti wakiwa kwenye makambi wakipata huduma

Waathirika wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Haiti wametoa siku sitini pekee kwa Umoja wa Mataifa UN kuanzisha mazungumzo nao juu ya kuwalipa fidia ya mabilioni ya dola na iwapo watashindwa kufanya hivyo watawafungulia kesi. Waathirika hao wa ugonjwa wa kipindupindu wamekuwa wakidai fidia kutokana na makosa yaliyofanywa na Umoja wa Mataifa UN ambao unatuhumiwa kuwa mstari wa mbele kupeleka vijidudu vinavyosababisha ugonjwa huo nchini Haiti.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Mataifa UN umeingia matatani kutokana na kutuhumiwa kuwaruhusu wanajeshi wake wa kulinda amani nchini Haiti kuchafua maji yanayotumiwa na wakazi hao kwa kuyawekea vijidudu vinavyosababisha ugonjwa wa kipindupindu.

Tuhuma hizo za wanajeshi wa kulinda amani nchini Haiti kuchafua maji hayo zilielezwa kuwa na ukweli uliothibitishwa na Wataalam wa Ugonjwa wa Kipindupindu katika Umoja wa Mataifa UN.

Licha ya Umoja wa Mataifa UN kupitia wataalam wake kukiri kuna uwezekano wa uwepo wa ukweli wa kuchafuliwa kwa maji hayo lakini umekaidi kulipa fidia kwa waathirika wa ugonjwa huo.

Umoja wa Mataifa UN umeendelea kusisistiza ilichokifanya ni kuwakinga waathirika hao kwa maradhi na hivyo wanaweza wakafuata njia za kisheria iwapo wanaona hawajatendewa haki na umoja huo.

Jopo la wanasheria wanaowatete waathirika hao limesema Umoja wa Mataifa UN umevunja sheria za kimataifa na hivyo watawasilisha mahakamani madai ya kulipwa fidia kwa wateja wao yenye thamani dola laki moja kwa familia ambazo ndugu zao walifikwa na mauti na dola elfu hamsini kwa kila mgonjwa.

Waathirika hao ni pamoja na watu elfu nane ambao ndugu zao walipoteza maisha kutokana na maradhi ya kipindupindu ambayo yanaelezwa chanzo chake ni Kambi ya Kijeshi ya Nepal na ndiyo yakaingia nchini Haiti.