BANGLADESH

Idadi ya watu waliopoteza maisha nchini Bangladesh kufuatia kuanguka kwa ghrofa imefikia zaidi ya watu 1000

Idadi ya vifo vilivyosababishwa na kuanguka kwa jengo la ghorofa nane nchini Bangladesh vimefikia zaidi ya elfu moja huku Kikosi cha Uokoaji kikiendele kuondoa vifusi vilivyosalia kuangalia iwapo kuna miili ya watu walionaswa.

Kikosi cha Uokoaji kikiendelea kupata miili zaidi ya watu waliopoteza maisha kwenye jengo la ghorofa nane nchini Bangladesh
Kikosi cha Uokoaji kikiendelea kupata miili zaidi ya watu waliopoteza maisha kwenye jengo la ghorofa nane nchini Bangladesh REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Jengo hilo la ghorofa nane lilikuwa na kiwanda cha nguo ambapo taarifa zinaeleza wakati linaanguka kulikuwa na watu zaidi ya elfu tatu ambao walikuwa kwenye taratibu zao za kazi za kila siku.

Kiongozi wa Kikosi cha Uokozi Brigedia Jenerali Siddiqul Alam Sikder amesema wanaendelea na operesheni yao kabambe kuhakikisha wanaondoa kifusi chote na takwimu zinaonesha miili iliyopatikana imefikia elfu moja na thelathini na tano.

Idadi ya miili imeongezeka kufikia zaidi ya elfu moja baada ya miili zaidi kupatikana usiku wa kuamkia leo wakati wanajeshi wakiendelea kuondoa vifusi vilivyosababisha na kuanguka kwa ghorofa hilo.

Msemaji wa Jeshi Kapteni Shahnewaz Zakaria amesema wataendelea na zoezi hilo hali kuhakikisha wameondoa kifusi chote na kutoa idadi ya miili itakayokuwa inapatikana pindi operesheni hiyo inavyoendelea.

Taarifa zinasema miili inayopatikana kwa sasa kwa kiasi kikubwa imebakia mifupa baada ya sehemu kubwa wa mwili kuharibika baada ya kunaswa kwenye kifusi kwa kipindi cha zaidi ya siku kumi na saba sasa.

Duru zinabainisha kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa miili zaidi ya watu walionaswa kwenye kifusi hicho na hivyo idadi ya watu waliopoteza maisha inaweza ikawa kubwa zaidi ya ilivyokuwa inakadiriwa.

Katika hatua nyingine Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Viwandani nchini Bangladesh wametaka serikali kusimama kidete kuhakikisha waathirika wote wanalipwa fidia haraka iwezekanavyo.

Rais wa Shirikisho hilo la Wafanyakazi Fermeture Usines amesema wao hawatokuwa tayari kuona waathirika wa ajali hiyo ya kuanguka kwa ghorofa hawalipwi fidia na iwapo itakua hivyo watakuwa tayari kuifikisha mahakamani serikali.

Viwanda vya Nguo nchini Bangladesh vimeendelea kuwa si sehemu salama kwa wafanyakazi wake kutokana na vingi vyao kukosa sifa zinazopaswa huku serikali ikishindwa kuchukua hatua ya kuvifungia.